Haya ndiyo matumizi sahihi ya ‘Earbuds’, kuepuka madhara

Dar es Salaam. Ikiwa unatumia vifaa vya kusikilizia sauti masikioni kama Earbuds unapaswa kujua mwongozo sahihi wa utumiaji ili kujiepusha na athari katika afya ya sikio.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), katika ripoti yake ya mwaka 2022 kuhusu usikivu salama, zaidi ya watu bilioni moja duniani wenye umri kati ya miaka 12 hadi 35 wako katika hatari ya kupoteza uwezo wa kusikia kutokana na kusikiliza sauti kwa kiwango kikubwa kupita kiasi kupitia vifaa binafsi vya sauti.

Shirika hilo pamoja na idara nyingine za kiafya kama Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kupitia taarifa yake ya mwaka 2023 inayohusu upotevu wa kusikia unaosababishwa na sauti, pamoja na utafiti kuhusu matumizi ya vijana na vifaa vya sauti ya mwaka 2019 uliofanywa na The BMJ Global Health yameeleza athari na miongozo ya kusikilizwa vifaa hivyo.

Mashirika hayo kwa pamoja yanaonya utumiaji usiozingatia usahihi unaweza kusababisha mhusika kupoteza uwezo wake wa kuisikia wa awali.

Ikumbukwe vifaa hivyo vinaingizwa ndani sikioni na vinatumika sana hasa kwa vijana ambao ndio watumiaji wakubwa wa simu janja ikiwamo kusikiliza muziki, kuangalia video hadi kupokea simu za kikazi, vifaa hivi vimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

Matumizi ya Earbuds yanahitaji umakini kidogo ili kulinda afya ya masikio yako na kuhakikisha kifaa chenyewe kinadumu. Ingawa ni teknolojia rahisi, kuna mambo ya msingi ya kuzingatia.

Kwanza unapaswa kufuata kanuni ya sauti (Volume Control) ya 60/60 ambapo inashauriwa kusikiliza muziki kwa sauti isiyozidi asilimia 60 ya uwezo wa kifaa chako.

Usitumie Earbuds kwa zaidi ya dakika 60 mfululizo bila kupumzika, kwani sauti kubwa kupita kiasi inaweza kusababisha upotevu wa usikivu wa kudumu.

Zingatia usafi na utunzaji wa vifaa hivyo kwani huingia ndani ya tundu la sikio, hivyo zinakusanya nta na bakteria kwa urahisi.

Unapaswa kusafisha mara kwa mara kwa kutumia kitambaa laini, kikavu, au tishu kusafisha sehemu ya nje.

Pia, ondoa nta kwa kutumia kijiti kidogo (kama kiberiti au brush laini) iliyoganda kwenye matundu ya spika, lakini fanya hivyo kwa umakini usitoboe chujio.

Kausha kabla ya kuchaji na kamwe usiweke Earbuds kwenye kasha lake la kuchaji zikiwa na unyevu au jasho.

Hata katika usalama wako wa mazingira kama barabarani unapaswa kuepuka kutumia Earbuds zote mbili unapotembea au kuendesha ni muhimu kusikia sauti za honi au dharura.

Hakikisha unatumia “Ear tips” (zile raba za ncha ya Earbuds) zenye saizi sahihi kwa sikio lako ili kuzuia sauti ya nje isivuje ndani, jambo ambalo hukufanya usihitaji kuongeza sauti sana.

Utafiti uliochapishwa mwaka 2019 katika jarida la The BMJ Global Health umebainisha vijana wengi hutumia vifaa hivyo kwa viwango vya sauti vinavyozidi 85, kiwango ambacho wataalamu wanasema kinaweza kusababisha uharibifu wa seli za ndani ya sikio, endapo kitadumu kwa muda mrefu.

Aidha, kwa mujibu wa CDC mwaka 2023, kelele za muda mrefu zinaweza kusababisha hali ya tinnitus (mlio wa kudumu masikioni) pamoja na kupungua kwa uwezo wa kusikia taratibu bila muhusika kugundua mapema.

Ikumbukwe teknolojia imeleta urahisi katika mawasiliano na burudani, lakini matumizi yake yanahitaji tahadhari.