Kuzimwa mtandao Gabon,  wanazuoni waonya wataka mbinu mbadala Afrika

Dar es Salaam. Wanazuoni wameyataka mataifa ya Afrika kubuni njia mbadala wa mitandao ya kijamii itakayoweza kudhibitiwa na viongozi wa nchi husika kabla ya kufikia uamuzi wa kufungia mitandao hiyo, ambayo imekuwa fursa ya kiuchumi na mawasiliano ya haraka duniani kote.

Wito huo wa wadau umekuja kufuatia hatua ya Gabon kutangaza kusitisha matumizi ya mitandao ya kijamii kwa madai ya kulinda maadili ya jamii dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao hiyo.

Uzimaji wa intaneti umeshamiri kwa mataifa ya Afrika nyakati za uchaguzi kwa madai ya kulinda amani na kuepusha upotoshaji.

Jumanne, Februari 17, 2026, Serikali ya Gabon, kupitia shirika lake la Mawasiliano la High Authority for Communication (HAC), imezima mitandao yote ya kijamii kwa kipindi kisichojulikana kwa madai ya kulinda heshima za watu, maadili ya umma na mshikamano wa kijamii dhidi ya matumizi mabaya ya majukwaa hayo.

Katika taarifa iliyotolewa na Msemaji wa HAC, Jean‑Claude Mendome,  kupitia  Shirika la Utangazaji la Taifa hilo, Radio Television Gabonaise (RTG) amesema hatua hiyo inalenga kudhibiti maudhui yanayoweza kuharibu heshima, kuchochea chuki au kusababisha migawanyiko katika jamii.

Nchini Gabon ambapo mitandao maarufu ya kijamii inayotumiwa ni pamoja na  WhatsApp, Facebook na TikTok, Serikali imesema imebaini inatumiwa vibaya, kinyume na sheria za Gabon na kanuni za kimataifa ikiwemo kuchochea vurugu za umma, kuenea kwa taarifa potofu na unyanyasaji wa mitandaoni ikiwatuhumu wamiliki na waanzilishi wa mitandao wameshindwa kudhibiti maudhui yasiyofaa.

Ukubwa wa tatizo kwa Afrika

Gabon inachukua uamuzi wa juu zaidi huku ikiangukia katika mwelekeo ulioshamiri barani Afrika, ambapo uzimaji wa mitandao ya kijamii kwa miaka ya hivi karibuni imekithiri ulijirudia mara kwa mara katika mataifa mbalimbali vipindi vya uchaguzi.

Katika vipindi vya uchaguzi mkuu, mataifa mengi ya Afrika yakiwemo Uganda, Tanzania, Niger, Zambia, DRC, Zimbabwe, Ethiopia, Guinea, Chad, Mali, Sudan na Gabon yenyewe yameshuhudia kuzima mitandao kwa siku kadhaa kwa madai ya kulinda amani wakati wa uchaguzi mkuu wa viongozi wa kitaifa.

Katika vipindi hivyo, Serikali zimekuwa zikisisitiza kuwa matumizi mabaya ya mitandao hiyo imekuwa chanzo cha kuchochea migawanyiko na migogoro hivyo kuathiri utulivu wa kisiasa, hata hivyo athari za uzimaji huo wa mitandao zimeendelea kuwa hasi mbali na kulinda amani.

Katika karne ya sasa, ambapo intaneti imepita matumizi ya anasa au burudani pekee,  mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Facebook, Instagram, X na TikTok,  imekuwa miundombinu muhimu inayogusa kila nyanja ya maisha ya binadamu  uzimaji wa mitandao umekuwa ukisababisha athari kubwa kwa wananchi na biashara ndogondogo.

Mtetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania, Dk Ananilea Nkya anasema kuzima mitandao ya kijamii kwa kulinda amani hakuna uhusiano akisisitiza kuwa amani haivurugiki kwa watu kuwa na njia za mawasiliano na kuonya kuwa kufanya hivyo, huondoa uhalali wa michakato ya kisiasa inayoendelea wakati jamii ikiwa haina mawasiliano.

“Amani haihusiani chochote na mitandao ya kijamii, kuzima mitandao hiyo ni kuwanyima watu haki ya kuwasiliana hasa kama kuna uchaguzi unafanyika, hiyo ni ishara tosha kuwa huo uchaguzi hauwezi kuwa huru na wa haki,” anasema.

Mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Azaveli Lwaitama anaongeza kufunga mitandao hiyo ni kuwarejesha wananchi zama za ukoloni kwa kuwanyang’anya uhuru wao wa kuchangamana na kuwasiliana bila vikwazo.

“Serikali inayozima mitandao ya kijamii inaonesha kuwa hao si viongozi wa kuwasaidia watu bali ni watawala, viongozi wanapaswa kuwasaidia watu siyo kuwadhibiti na kuwatawala. Kuwazimia mitandao watu na kuwapa ugumu wa kuwasiliana na kupata taarifa ni kuwarudisha zama za ukoloni,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu uzimaji mitandao ya kijamii uliofanywa na Gabon, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo, amebainisha licha ya changamoto za mitandao hiyo, kabla ya kuamua kuizima inapaswa kuandaliwa mbadala wake ili kulinda fursa zake zikiwemo kupata taarifa muhimu za kimataifa zinazosambaa kwa kasi mitandaoni.

“Tofauti na nchi zetu, Taifa la China halitumii Google, wanatumia mtandao wao mwingine, hawatumii Whatsapp wanatumia Wichat, lakini wanapoona madhara kwenye mtandao fulani ambao hawana uwezo wa kuudhibiti wanaita wataalamu wao kuanzisha mtandao wao wa huduma kama hiyo kisha huo wanaufunga,” amesema.

Mwanazuoni huyo amesema badala ya kuwaondolea wananchi huduma za mitandao mbadala wake unapaswa kuandaliwa kabla, huku akitaja njia za kulinda maadili na matumizi sahihi ya mitandao hiyo badala ya kuifuga.

“Tunatakiwa kujiuliza, tunazima mtandao kulinda maadili au kuwazuia watu kuwasiliana, kama ni maadili na matumizi tunaweza kulinda hayo bila kuizima ikiwamo kuwekeza kwenye elimu ya matumizi sahihi ya mitandao shuleni kama sehemu ya mtaala na kufanya warsha, mafunzo na matangazo kwenye vyombo vya habari kuhusu matumizi sahihi ya mitandao hii badala ya kuifunga.