Februari ni mwezi wa vigogo kuiaga dunia. Hivyo ndivyo unavyoweza kuuelezea mwezi huo kutokana na vifo vingi vya viongozi wa kitaifa kutokea katika mwezi huo na kuacha simanzi kwa familia na taifa kutokana na vifo vyao.
Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi 2026, ni dhahiri kwamba Februari imechukua maisha ya waliowahi kuwa viongozi mashuhuri hapa nchini, miongoni mwa Watanzania wengine waliopoteza maisha.
Kinachoshangaza zaidi, kwanini Februari? Licha ya kwamba viongozi wengine walifariki katika miezi tofauti, Februari imechukua wengi katika kipindi hicho huku jambo hilo likibaki kuwa fumbo kuu.
Hata hivyo, baadhi ya wadau wanaeleza kwamba suala hilo ni mgongano wa matukio usio na chochote nyuma yake, kwani wakati mwingine matukio ya kufanana hutokea kwa wakati mmoja bila kutarajia.
Katika makala haya, Mwananchi linaangazia baadhi ya vigogo waliofariki dunia Februari pekee huku kukiwa na sintofahamu kwenye jambo hili zikiwa zimesalia siku 10 kumaliza mwezi huu na rekodi kama hiyo.
Februari 29, 2024, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alitangaza kifo cha Mzee Ali Hassan Mwinyi (98), Rais wa Serikali ya awamu ya pili.
Mzee Ali Hassan Mwinyi (98), Rais wa Serikali ya awamu ya pili.
Mzee Mwinyi alifariki dunia saa 11 jioni katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam. Alikuwa akipatiwa matibabu tangu Novemba 2023 huko London, Uingereza na baadaye kurejea nchini na kuendelea na matibabu katika Hospitali ya Mzena.
Mzee Mwinyi alifariki dunia akiwa na miaka 98. Mei 8, 1925, ndio tarehe ambayo Mwinyi alizaliwa katika Kijiji cha Kivure, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. Machi 2, 2024, Mzee Mwinyi alizikwa nyumbani kwake, Mangapwani, Unguja visiwani Zanzibar.
Februari 17, 2021, mwanasiasa mkongwe wa upinzani visiwani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kabla ya kujiunga na ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad.
Mwili wa Maalim Seif, ambaye alikuwa kiongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kabla ya kujiunga na ACT Wazalendo, ulizikwa Februari 18, 2021 kisiwani Pemba.
Enzi za uhai wake, Maalim Seif alikuwa kinara wa siasa za upinzani Zanzibar ambapo kupitia mazungumzo ya mwafaka kati yake na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, walifanya marekebisho ya Katiba kuruhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Kama ilivyokuwa kwa Maalim Seif, Februari 17, 2021, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi alifariki dunia jijini Dodoma katika hospitali ya Benjamin Mkapa baada ya kuugua ugonjwa wa moyo. Alizikwa Februari 20, 2021 katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi.
Wakati wa uhai wake, moja ya sifa kubwa aliyopewa ni pamoja na kuwalea watumishi wa umma hasa makatibu wakuu wote kwa usawa, bila upendeleo wowote.
Pia, inaelezwa kwamba Kijazi alikuwa mtu makini katika kazi kwa sababu alikuwa na uwezo wa kuchanganua mambo katika muktadha wake, jambo ambalo liliwashangaza wengi.
Februari 10, 2024, Taifa lilimpoteza Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyefariki dunia katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu kwa maradhi ya shinikizo la damu, matatizo ya mapafu na kujikunja kwa utumbo.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Miaka miwili imetimia sasa tangu Lowassa alipofariki dunia, akiacha kumbukumbu ya uongozi uliotukuka na mfano wa kuigwa kwa viongozi vijana wa sasa.
Lowassa alizikwa Februari 17, 2024 huko Monduli, Arusha akiacha kumbukumbu ya kiongozi mwenye uwezo wa kufanya mambo yatokee. Alikuwa mwanasiasa mwenye ustahimilivu na busara katika uongozi wake.
Mwingine aliyefariki dunia Februari ni Waziri wa zamani wa Katiba na Sheria, Bakari Mwapachu ambaye alifariki dunia Februari 12, 2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu.
Waziri wa zamani wa Katiba na Sheria, Bakari Mwapachu
Mwapachu alikuwa Mbunge wa Tanga kuanzia mwaka 2000 hadi 2010 alipomwachia kijiti Omar Nundu (marehemu) na amewahi kushika nafasi za mbalimbali za uongozi serikalini katika vipindi tofauti.
Safari yake ya kimaisha iliyoanza Julai 25, 1939, ilifikia tamati Februari 12, 2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam. Mazishi ya kiongozi huyo yalifanyika Februari 13, 2021 kijiji cha Pande Wilaya ya Tanga.
Februari 15, 2021, taifa lilimpoteza mwanasiasa mkongwe, Dk Muhammed Seif Khatib (70), aliyefariki dunia Februari 15, 2021 asubuhi mjini Unguja. Dk Khatib alizikwa siku iliyofuata huko Mpendae, Unguja.
Waziri wa zamani Dk Muhammed Seif Khatib afariki dunia
Dk Khatib ni mwanasiasa aliyekuwa mbunge wa jimbo la Uzini, Unguja na amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM na nafasi kadhaa uwaziri kama vile Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Atakumbukwa kwa utaalamu wake wa lugha ya Kiswahili ambapo hadi anafariki dunia alikuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza).
Mbali na vigogo hao, Februari 7, 2025, mwanasiasa mkongwe nchini, Nicodemus Banduka (80) alifariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mloganzila iliyopo jijini Dar es Salaam.
Banduka aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Shinyanga, Pwani na Mjumbe wa kamati kuu Taifa ya CCM. Pia, alikuwa mmoja wa watu walioanzisha CCM baada ya muungano wa vyama vya ASP na Tanu.
Banduka alikuwa miongoni mwa wajumbe 10 wa Tanu, ambapo mwenyekiti wao alikuwa Peter Kisumo, na wajumbe 10 kutoka ASP, mwenyekiti wao akiwa Sheikh Thabit Kombo, walioteuliwa kuunganisha vyama hivyo.
Wadau wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu vifo vya vigogo hao kutokea Februari ambapo wanaeleza kuwa ni jambo la kawaida kwa hali kama hiyo kutokea, mwezi mmoja ukawa na watu wengi wa aina fulani.
“Mimi naliona ni jambo la kawaida tu, imetokea tu kwamba wengi wamefariki dunia Februari, nina uhakika ukiamua kufuatilia vizuri hata mwezi mwingine utapata wengine wengi tu, inatokea,” anasema Gilbert Mwakibinga, mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam.
Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Nestory Sungura anasema ni jambo la kushangaza kwa vifo hivyo, tena vya watu mashauhuri kutokea mwezi mmoja, miaka tofauti, na ni vigumu kujua siri iliyo nyuma yake.