ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Abdihamid Moallin ‘Master Lecturer’, huenda akarejea Tanzania hivi karibuni ikiwa atafikia makubaliano na timu tatu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, baada ya kuonyesha uhitaji mkubwa kwa kocha huyo.
Kocha huyo mwenye uraia wa Marekani akiwa na asili ya Somalia, kwa sasa yupo mapumziko Marekani tangu alipoachana na Yanga Julai 27, 2025, akiwa ni Mkurugenzi wa Ufundi, ingawa huenda muda wowote akarejea nchini ikiwa mazungumzo na timu hizo yatafikiwa ipasavyo.
Hata hivyo, Mwanaspoti limepenyezewa taarifa zikieleza miongoni mwa timu zinazofanya mazungumzo na Moallin, kimya kimya ni TRA United inayonolewa na Mrundi Etienne Ndayiragije, ambaye hadi sasa kumekuwa na sintofahamu juu ya kibarua chake.
Ndayiragije aliyejiunga na timu hiyo baada ya kuachana na Kenya Police FC ya Kenya, Oktoba 29, 2025, baada ya kuipa pia ubingwa wa Ligi ya Kenya, inadaiwa hana uhusiano mzuri na mabosi wa TRA, jambo linalofungua mazungumzo hayo na Moallin.
Kocha huyo aliipa Kenya Police ubingwa huo ukiwa ni wa kwanza kwa kikosi hicho katika historia tangu kilipopanda daraja mwaka 2021, hivyo, kuzima utawala wa Gor Mahia iliyochukua mara mbili mfululizo kuanzia msimu wa 2022-2023 na 2023-2024.
Moallin aliyewahi kuifundisha Azam FC na KMC, inaelezwa anafanya mazungumzo na timu tatu za Tanzania, ambazo hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu TRA United ni miongoni mwao, licha ya usiri uliotawala wa kutotaka kuweka wazi nyingine kwa sasa.