Mabosi Azam washtukia ishu ya Ibenge, wamuwekea ngumu

UONGOZI wa Azam FC, umeweka wazi hauko tayari kumuachia kocha mkuu wa timu hiyo, Florent Ibenge aondoke ndani ya kikosi hicho kwa sasa, licha ya kuzuka pia kwa taarifa zikidai Mkongomani huyo anawindwa na Shirikisho la Soka la Angola (FAF).

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu Msaidizi wa Azam, Rashid Seif, amesema kocha huyo bado wana malengo naye makubwa kwa sasa kikosini, hivyo taarifa zote zinazomuhusisha kuondoka sio za kweli, kwani wanaamini ni mtu sahihi kwao.

“Nikuhakikishie ndugu yangu, Ibenge haendi popote na hatuko tayari kuona hilo likitokea, ni kocha mzuri na tumeona kile alichofanya katika timu kwa muda mfupi, malengo yetu ni kujenga kikosi cha ushindani kupitia uwepo wake,” amesema Seif.

Vyanzo mbalimbali vinadai Shirikisho la Soka la Angola (FAF), linamuona Ibenge ni chaguo sahihi katika kikosi hicho kwa sasa, baada ya aliyekuwa kocha wa timu ya taifa, Mfaransa Patrice Beaumelle, kuondoka kwa makubaliano ya pande mbili.

Hata hivyo, licha ya juhudi za shirikisho hilo, uongozi wa Azam hauko tayari kumwachia Ibenge kutokana na kuiandikia rekodi ya kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza msimu huu, tangu timu hiyo ilipoanza kushiriki mwaka 2013.

Azam FC iliandika historia mpya katika Michuano ya CAF, baada ya timu hiyo kuandika rekodi ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa Julai 23, 2004 ikifahamika kwa jina la Mzizima FC.

Matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam, waliopanda rasmi Ligi Kuu Julai 27, 2008, wameweka historia mpya tangu kuanzishwa kwake chini ya Kocha Mkuu, Mkongomani Florent Ibenge aliyejiunga nao Julai 5, 2025, akitokea Al Hilal Omdurman ya Sudan.

Ibenge aliyechukua nafasi ya Mmorocco, Rachid Taoussi, aliiwezesha pia Azam kumaliza nafasi ya tatu kundi B la Kombe la Shirikisho Afrika na pointi tisa, ikiwa ni rekodi kwa timu za Tanzania kuzikusanya katika ushiriki wake wa kwanza CAF.

Azam imemaliza na pointi hizo nyuma ya vinara, Wydad Casablanca (Morocco) iliyokusanya 15 na AS Maniema Union (DR Congo) yenye 12, zikiwa ni nyingi, kwani hata Yanga, Simba na Namungo FC hazijazifikia katika ushiriki wao wa kwanza wa CAF.