Dar es Salaam. Wakati mashahidi wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu wakieleza walivyokamatwa kwa kuhamasisha kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, mshtakiwa huyo amewahoji iwapo walishtakiwa na nani anayewahudumia jijini Dar es Salaam.
Mashahidi hao ambao ni miongoni mwa mashahidi fiche (waliolindwa, yaani wasiotakiwa kuonekana wala kutambulika), wanaotoa ushahidi wakiwa ndani ya kizimba maalumu ambamo hawawezi kuonekana kwa wasikilizaji wala mshtakiwa, isipokuwa kwa majaji tu wametambulishwa kwa majina ya P4 (29) na P7 wakazi wa Arusha.
Shahidi P4 alitoa ushahidi wake Februari 17 jioni na P7 ametoa ushahidi leo Jumatano, Februari 18, 2026.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusu kusudio la kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kesi hiyo inasikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Shahidi P4 ambaye ni shahidi wa 10 wa upande wa mashtaka katika ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala amesema yeye ni dereva bajaji anayefanyia shughuli zake eneo la kwa Mromboo.
Kwa mujibu wa ushahidi huo, Aprili 3, 2025, saa sita mchana wakati akimsubiri mteja, kupitia simu yake aliingia katika mtandao wa Youtube akakutana na habari za mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, katika video ambayo ilikuwa inahamasisha kuzuia kufanyika kwa uchaguzi.
Katika video hiyo pamoja na maneno mengine Lissu alisikika akitamka kuwa:
“Hata uende wapi huwezi kupata haki, hata majaji ni vibaraka wa CCM, hata tume ndogo ya uchaguzi ilipanga kuvuruga uchaguzi wa Serikali wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka 2024 uliondoa viongozi wao (Chadema). Watafanya uasi, watakinukisha.”
Hivyo kutokana na ugumu wa kimaisha maneno hayo ndio yaliyomfanya ashawishike na maneno ya Lissu.
Baada ya kupata abiria aliwapeleka kwa Mromboo na aliporudi katika kijiwe chao cha Bajaji, alikuta mada ile ya kauli za Lissu kuhusu kukinukisha na watu wengi walikuwa wakiunga mkono, wakisema bora kinuke unafuu wa maisha unaweza kuwepo.
Baada ya dakika 20, alidai walitokea Polisi na watu waliokuwepo eneo lile walianza kukimbia ndipo yeye na mwenzake P7 walikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi Muriet.
Baada ya kufikishwa kituo cha Muriet, walikaa kwa saa moja na kisha kupelekwa kituo Kikuu cha Polisi, mjini ambako walielezwa makosa yao kuwa ni kupanga kuzuia uchaguzi.
Alidai yeye na mshtakiwa mwenzake P7 waliandikwa maelezo na kupelekwa rumande mpaka kesho yake alipowekewa dhamana na mdogo wake na Aprili 17, 2025 aliporudi kuripoti kituoni hapo ndipo akaandikwa maelezo yake.
Kwa upande wake shahidi P7, ambaye ni shahidi wa 11, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Tawab Issa, ameeleza kuwa ni dereva bajaji katika eneo hilo la kwa Mromboo.
Kwa mujibu wa ushahidi wake Aprili 3, 2025, jioni akiwa kijiweni hapo, wakiwa katika mazungumzo ya kawaida kuna mwenzao mmoja akawauliza kama walikuwa wamesikia Chadema wanapanga kuzuia uchaguzi wa mwaka huo, huku akiwaeleza Lissu aliyokuwa ameyazungumza.
Maneno hayo ni pamoja na kwamba: “Polisi wanaiba kura na hata wakienda mahakamani hawatapata haki kwa sababu majaji ya watu wa CCM. Mwaka 2024 Tume ya Uchaguzi ilipewa maelekezo ya kukata wajumbe wa Chadema.
Hivyo maneno hayo yalimpa hamasa na kwa kutumia simu yake akaingia katika mtandao wa Youtube kujiridhisha, akafungua akamsikiliza Lissu akitamka maneno hayo.
Pia shahidi huyo amesimulia walivyokamatwa na mwenzake mpaka Aprili 17 alipochukuliwa tena maelezo.
Baada ya kumaliza ushahidi wao huo wa msingi, mashahidi hao wamehojiwa na mshtakiwa Lissu maswali mbalimbali ya dodoso, ambapo kwa nyakati tofauti, walisema licha ya kukamatwa na Polisi, hawakuwahi kushtakiwa.
Lissu: Waeleze majaji kama kumuunga mkono Tundu Lissu ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi hii.
Shahidi: Mimi sio mwanasheria
Lissu: Kwani kuzuia uchaguzi ni kosa kwa mujibu wa Sheria?
Shahidi: Ni kosa, ndio maana tulikamatwa
Lissu: Waeleze majaji kama ulipelekwa mahakamani kwa kosa la kutaka kufanya fujo.
Shahidi: Sijapelekwa mahakamani
Lissu: Waeleze majaji kama baada ya kuchuliwa maelezo, kama hao mapolisi walihangaika na wewe kwa kosa la kufanya fujo.
Shahidi: Ndio maana nilikuwa naenda kuripoti polisi.
Lissu: Ulivyokuwa unaenda kuripoti polisi, walikuwa wanakwambia nini?
Shahidi: Nilikuwa naambiwa nifagie uwanja nje na kisha nasaini na kuondoka. Ndiyo maana nimefika hapa.
Lissu: Umefika hapa kwa sababu yangu mimi.
Shahidi: Kosa lako, wewe ndio umenisabishia mimi kufika hapa.
Lissu: Waeleze majaji umekujaje leo hapa mahakamani?
Lissu: Kutoka Kirai (Arusha) hadi hapa Dar umekuja kwa miguu?
Lissu: Nani amekupa nauli?
Lissi: Nani anakupa hela ya chakula na sehemu ya kulala?
Shahidi: Nimeshakueleza ni mwanamke wangu, eeh.
Lissu: Je, umewahi kutishiwa maisha na kiongozi au mfuasi au mwanachama yoyote wa Chadema, kuhusiana na kesi hii?
Shahidi: Sijawahi kutishiwa, huwezi kutishiwa kama haujulikani.
Lissu: Je, umewahi kutishiwa kuharibiwa bajaji yako?
Shahidi: Bro wewe maswali yako mbona nimeshajibu.
Lissu: Unajua kwa nini umepewa jina la P7
Shahidi: Ndiyo najua, ni kuficha jina langu kwa sababu ya usalama wangu.
Lissu: Shahidi umeieleza Mahakama wewe unakaa Arusha, waeleza majaji, hapa Dar es Salaam umekuja lini?
Lissu: Waeleze majaji, nani amekwambia uje Dar es Salaam.
Shahidi: Nashindwa kusema.
Shahidi: Ninazo sababu binafsi.
Lissu: Tuambie tu, maana hapa hakuna anayekuona ni majaji pekee yao ndio wanakuona.
Shahidi: Nilipigiwa simu na wakili wa Serikali.
Lissu: Nani aliyekulipia nauli yako kutoka Arusha mpaka Dar es Salaam?
Shahidi: Nilijilipia mwenyewe kwa sababu nilikuwa na shughuli zangu binafsi.
Lissu: Siku ya Aprili 3, 2025 uliandika maelezo polisi yalihusu kosa gani?
Shahidi: Kwanza walitwambia tuna kesi ya kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Lissu: Ulipelekwa mahakamani?
Shahidi: Sikuwahi kupelekwa mahakamani.
Lissu: Waeleze majaji hiyo kesi ya kuzuia uchaguzi iliishia wapi?
Lissu: Sasa shahidi nikikwambia ulikamatwa bure tu kwa sababu ya kuzuia uchaguzi wala sio kosa, utasemaje?
Lissu: Kuzungumza hayo maneno (kuzuia uchaguzi), kuunga mkono ni kosa la jinai?
Shahidi: Kwa sababu mimi sio msimamizi wa sheria, siwezi kujua
Lissu: Kwa kauli kwamba majaji ni vibaraka wa CCM ni kosa la jinai?
Lissu: Na kusema mapolisi wanaiba kura, ni kosa la jinai?
Lissu: Waeleze majaji kama una fahamu neno kunuka
Shahidi: Kunuka ni kitu kinachotoa harufu mbaya
Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu neno kunukia?
Shahidi: Kunukia ni kitu kinachotoa harufu nzuri.
Lissu: Mtu akisema nitakinukisha, maana yake atakifanya kitoe harufu mbaya.
Shahidi: Inategemeana unazungumza katika maana ipi, lakini kwa lugha zinazotumika mtaani ni kufanya vurugu.
Lissu: Mtaani wapi, mimi sijawahi kusikia mtaani kwangu.
Shahidi: Mtaani kwetu tunazungumza hivyo.
Lissu: Umewahi kuwasiliana na kiongozi yoyote wa Chadema?
Lissu: Umewahi kutishiwa maisha na kiongozi yoyote wa Chadema au mwachama au mfuasi aliyekutishia kukudhuru kwa sababau wewe ni shahidi?
Lissu: Waeleze majaji kama kuna kiongozi yoyote wa Chadema, au mwanachama au mfuasi aliyetishia kuharibu mali zako au kumtishia ndugu yako kwa aina yoyote ile kwa sababu ya kesi hii.
Lissu: Waeleze majaji sababu ya wewe kutoa ushahidi ukiwa umejificha katika hizo mbao (kizimba maalumu).
Shahidi: Nahofia maisha yangu pia.
Lissu: Nani aliyekufundisha hayo maneno wakati hujatishwa?
Shahidi: Sijasema kutishiwa maisha.