ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wilfred Kidao, ni miongoni mwa wajumbe nane wanaounda Bodi ya Usimamizi wa TRA United SC inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Edmund Kawamala.
Bodi hiyo imezinduliwa leo Februari 18, 2026 na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda, katika ofisi za TRA Dar es Salaam, na kuitaka kuisimamia kikamilifu timu hiyo na kuifanya kuwa bora na tishio katika michuano ya ndani na kimataifa.
Pamoja na mambo mengine, ameisisitiza kwenda kusimamia nidhamu ya timu ili kuifanya kuwa ya mfano dhidi ya klabu zingine zinayoshiriki michuano mbalimbali hapa nchini.
Amesema, dhamira ya TRA kuianzisha timu hiyo mbali na kutoa burudani, imelenga kupeleka ujumbe kwa wananchi juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari jambo ambalo ndiyo msingi wa ukuaji wa uchumi wa nchi huku akitarajia matokeo chanya katika jambo hilo mara baada ya kuanzishwa kwa Bodi hiyo.
“Tumetengeneza timu kwa sababu dhamira yetu kubwa ni kwenda kufungamanisha wajibu wa TRA na ushiriki wa moja kwa moja wa wananchi katika kuelewa umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari, hivyo imani yangu nyinyi kama Bodi mtakwenda kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wananchi wanaliona suala la kulipa kodi kama jukumu lao na siyo vinginevyo,” amesema Mwenda.
Amesema anatambua umuhimu wa suala la michezo nchini, hivyo kupitia timu hiyo pamoja na Bodi iliyoundwa matarajio yao ni kwenda kuwa kioo cha michezo nchini ikiwa ni pamoja na kutoa taswira kwa wachezaji hususani kutoka nje ya nchi kuchangia kodi kutoka katika mishahara wanayolipwa.
Kamishna Mwenda amesema ili kufikia malengo ya Dira ya Mwaka 2050, TRA ikiwa ndiyo injini katika dhamira ya kufikia kiwango cha pato la taifa, wana wajibu wa kuhakikisha wanatumia njia mbalimbali za ukusanyaji wa mapato ikiwamo kupitia sekta hiyo ya michezo, jambo analoamini kuwa kama bodi hiyo itaweza kutumia weledi wao kuisimamia timu hiyo wanaweza kufanikiwa kama ilivyo matarajio yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TRA United SC, Edmund Kawamala, pamoja na mambo mengine amempongeza Kamishna Mwenda kwa wazo lake la kuianzisha timu hiyo ambayo matarajio yake itakuwa kuwa moja ya timu tishio ya mpira wa miguu barani Afrika.
Amesema wakiwa kama Bodi, watahakikisha wanafanya kila linalowezekana kuiwezesha timu hiyo kupeleka ujumbe wa kulipa kodi kwa wananchi, wakiamini asilimia kubwa ya wananchi wanapenda michezo, hivyo kupitia TRA United SC, wananchi watapata elimu ya kodi.
Mbali na Kidao, wajumbe wengine wa bodi hiyo ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, Angelina Ngalula, Juma Kisongo, Kamna Shomari, Zahoro Salum, Paul Walalaze na Elikunda Mndeme ambao ni watumishi wa TRA huku nafasi ya mjumbe wa mwisho ikitarajiwa kujazwa wakati wowote.
Kidao aliyedumu kwenye nafasi ya Katibu Mkuu wa TFF kwa miaka minane tangu alipoteuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 akiwa amekaa kwenye kiti hicho kwa mihula mitatu tofauti ya uongozi wa Karia ndani ya shirikisho hilo, mkataba wake ulifikia tamati Septemba 30, 2025.