Mapya yaibuka mgogoro wa uongozi CUF

Dar es Salaam. Ni nadra kuona ofisi za vyama vya upinzani zikilindwa na walinzi kutoka kampuni binafsi, lakini kwa sasa katika makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF) yaliyopo Buguruni, jijini Dar es Salaam si jambo la kushangaza kuwaona wakitanda kila kona wakifanya doria.

Hatua hiyo imegeuka shubiri kwa wanachama na wajumbe wa Baraza Kuu wanaounga mkono uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea na shughuli zao, kwa kuwa wanaonekana kama wageni na kujikuta wakikaa chini ya miti kama wanamsubiri mwenyeji aje kuwafungulia.

Magumu hayo yanawakuta hata makada waliokuwa wanalinda majengo ya ofisi hizo nao kwa sasa thamani yao inaonekana kama imeshuka.

Hali hiyo inajiri wakati chama kikiwa kimegawanyika katika makundi mawili; kundi linalodai linaelekea mahakamani kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, huku lingine likiwa katika maandalizi ya kufanya mkutano wa kuchagua uongozi mpya.

Chanzo cha mgawanyiko huo ni uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kutengua uchaguzi uliofanyika mwaka 2024 na kumrejesha madarakani Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti, pamoja na wenzake watano.

Mbali na Profesa Lipumba, wengine walioathirika na uamuzi huo ni Makamu Mwenyekiti Mbarouk Seif Salim (Zanzibar), Othman Dunga (Bara), Katibu Mkuu Husna Mohamed Abdallah, Naibu Katibu Mkuu Magdalena Sakaya (Bara) na Ali Juma Khamis (Zanzibar).

Sababu ya kutengua uchaguzi huo uliowaweka madarakani ni kwamba washindi hawakupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa na wajumbe, kinyume na matakwa ya katiba ya chama, inayohitaji mshindi kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura halali; hivyo mchakato ulipaswa kurudiwa.

Kufuatia uamuzi huo, wanachama wa chama hicho wamegawanyika katika makundi mawili, wale wanaopinga uamuzi wa Msajili na kuandaa kwenda mahakamani wakidai hatua hizo zilichukuliwa bila kuzingatia haki, ikiwamo haki ya kusikilizwa na wanaounga mkono uamuzi huo.

Wajumbe wa baraza kuu upande unaounga mkono upande wa Msajili wamewasili kwa ajili ya maandalizi ya kikao kinachotarajiwa kufanyika muda mfupi ujao, kwa lengo la kuandaa hoja na ajenda za Mkutano Mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumamosi ya wiki hii kwa ajili ya kuchagua uongozi mpya.

Katika makao makuu ya chama hicho, baadhi ya makada wamekusanyika nje huku ofisi zikiwa zimefungwa huku wanaounga mkono uamuzi wa Msajili wanaendelea na maandalizi ya uchaguzi huo, lakini hawawezi kuingia katika ofisi za chama kwa kuwa zimefungwa.

Hali hiyo ni tofauti na ilivyozoeleka, kwa kuwa, kawaida ofisi hizo huwa wazi. Hata hivyo, leo hali imebadilika ghafla.

Awali, ulinzi ulikuwa ukifanywa na makada wa chama, lakini sasa wamewekwa walinzi kutoka kampuni binafsi ya ulinzi waliovalia sare za njano kulinda ofisi hizo.

Walinzi hao wamejipanga katika geti kuu na geti dogo, huku wakifanya doria kuhakikisha hakuna mali inayotolewa wala mlango unaofunguliwa.

Sehemu ambazo hazijafungwa ni Ukumbi wa Shaban Mloo na ofisi ya walinzi wa chama hicho.

Hata hivyo, taswira ya ndani ya ofisi hizo imeonekana kuwa ya kawaida. Tofauti na siku nyingine, hakukuwa na hekaheka za watu kuingia na kutoka katika ofisi ya Mwenyekiti na viongozi wengine.

Majibu ulinzi kampuni binafsi

Akizungumzia uamuzi wa kuweka kampuni binafsi ya ulinzi leo Jumatano Februari 18, 2026, Dunga amesema: “Tumeweka ulinzi kwa sababu ya kulinda mali za chama. Waswahili wanasema kufa kufaana; walinzi wetu wa ndani hatuwaamini, wanaweza kutumia mgogoro huu kujinufaisha kwa kuchomoa vipuri.”

Amesema kuweka kampuni binafsi ya ulinzi ni salama zaidi, kwani iwapo kutatokea uharibifu au wizi, itakuwa rahisi kuwawajibisha kuliko ilivyo kwa makada wa chama.

“Kipindi kama hiki cha mpito baadhi wanaweza kutafuta faida binafsi, lakini tumeweka ulinzi kwa nia njema kabisa, kulinda mali za chama,” amesema.

Kundi linalounga mkono uamuzi wa Msajili linaendelea na jitihada za kutafuta akidi ya wajumbe. Kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, kuna wajumbe halali 43, na ili mkutano huo uwe halali, angalau wajumbe 25 wanapaswa kushiriki.

Hivyo, jitihada zinazoendelea zinalenga kuhakikisha idadi ya wajumbe inafikia angalau 25 ili waweze kufanya mkutano wa kupitisha hoja na majina ya wagombea wa nafasi za Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara na Makamu Mwenyekiti Zanzibar.

Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza kama anajua kuna uchaguzi huo, katika majibu yake amesema hajuhi chochote isipokuwa anasubiri kupewa taarifa.

“Hadi sasa sijui chochote isipokuwa nasubiri waniletee taarifa, ndipo tutawapa utaratibu namna mchakato wa Uchaguzi huo unavyotakiwa kufanyika na unatakiwa kuanzia wapi,” amejibu Nyahoza.