Manispaa ya Musoma yaazimia kuongeza ufaulu hadi asilimia 95

Musoma. Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara imejiwekea malengo ya kuongeza ufaulu kwa shule za sekondari kutoka asilimia 87 hadi 95 ikiwa ni sehemu ya kampeni yake ya kutokomeza daraja sifuri.

Katika mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka 2025, jumla ya wanafunzi 369 walipata daraja sifuri huku 288 wakipata daraja la kwanza kati ya wanafunzi 2,914 waliofanya mtihani huo katika manispaa hiyo.

Hayo yamebainishwa mjini Musoma leo Jumatano Februari 18, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka kwenye hafla ya kutoa tuzo na zawadi kwa walimu, mwanafunzi na shule zilizofanya vizuri kwenye zilizotolewa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Agnes Marwa.

Chikoka amesema kampeni hiyo pia inalenga kupunguza daraja la nne na kuongeza daraja la kwanza na la pili ambapo mikakati kadhaa imewekwa ili kuyafikia malengo hayo, ikiwa ni pamoja na kutokomeza utoro wa jumla na rejareja.

“Mwakani hatutaki lugha ya daraja sifuri, tayari tumekubaliana suala la chakula cha mchana ni lazima, tumeunda kamati kwa ajili ya kuangalia na kuweka utaratibu upi utumike na kiasi gani kitolewe ila suala la kuchangia chakula shuleni ni lazima,” amesema.

Amesema mkakati mwingine ni pamoja na kuanzisha tuzo za elimu katika Manispaa hiyo ambapo kutakuwepo na ushindani kati ya kata, shule walimu na wanafunzi lengo likiwa ni kuboresha elimu na ufaulu kwa ujumla.

Akizungumzia lengo la kutoa tuzo na zawadi hizo, Marwa ni kuwapa motisha walimu  waendelee kutimiza wajibu wao ili kuinua kiwango cha elimu katika Manispaa ya Musoma na mkoa kwa ujumla.

Amesema ni ukweli usiopingika kuwa masilahi ya walimu ni madogo ikilinganishwa na majukumu yao pamoja na hali ya maisha, hivyo wadau wanapaswa kutambua umuhimu wao kwa kuwapa motisha mbalimbali ili waendelee kutimiza wajibu wao.

“Mimi nitaendelea kuzungumza kuhusu masilahi ya walimu kila nitakapopata nafasi kule bungeni, natambua yapo maboresho yamefanyika kuhusu masilahi ya walimu lakini bado mahitaji ni makubwa maboresho zaidi yanahitajika, hivyo niahidi mimi nitakuwa balozi wa masilahi yao bungeni,” amesema.

Mbunge huyo amesema Mkoa wa Mara bado haufanyi vizuri katika matokeo ya mitihani ya kitaifa hivyo ni jukumu la kila mdau kuhakikisha anashiriki katika kukwamua sekta hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Hizi tuzo zitakuwa endelevu na niwaahidi kila mwaka thamani ya zawadi itakuwa ikiongezeka mara tatu kwa hiyo nitoe rai kwenu walimu kafanyeni kazi kwa weledi na kujituma zaidi, ili tuboreshe elimu ambayo ndiyo ufunguo wa maisha,” ameeleza

Wakizungumza baada ya kupokea tuzo na zawadi hizo baadhi ya walimu wamesema ili kufikia malengo hayo suala la ushirikiano baina ya Serikali, jamii na walimu ni la muhimu.

Mkuu wa Shule ya Ufundi Musoma, Gabriel Magita amesema changamoto kubwa hivi sasa ni ushirikiano hafifu kati ya jamii na shule hali ambayo kwa namna moja ama nyingine inasababisha ufaulu duni wa wanafunzi.

“Mwalimu unampa mwanafunzi kazi ya nyumbani ila akifika nyumbani anakosa usimamizi wa mzazi, kwa hiyo kazi haifanyiki na hata suala la utoro wa rejareja na jumla, pia, linatokana na kutokuwajibika kwa wazazi, kwa hiyo hapa unaweza kuona ushirikiano mzuri ulivyo na matokeo chanya katika kuboresha ufaulu,” amesema Magita.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyamitwebiri, Moja Mwangu amesema jamii inatakiwa kushiriki kikamilifu katika kufanikisha kampeni hiyo ya kutokomeza daraja sifuri.