Dar es Salaam. Wafanyakazi wa ndani ‘ma- house girl’ au mayaya, wameanzishiwa mafunzo ya ngazi ya diploma yatakayowawezesha kuwa na elimu ya namna ya kulea watoto, wazee, kuandaa vyakula na kutandika vitanda.
Mtalaa huo kwa wadada wa kazi umeanzishwa ili kupambana na changamoto kadhaa ikiwamo ya kukosa weledi wa namna ya kufanya kazi zao.
Kuanzishwa kwa mafunzo hayo ya ngazi ya diploma kutaongeza hadhi ya kazi hiyo kwa kuwa miongo iliyopita, kazi za ndani zimekuwa zikifanywa kimya kimya bila mikataba thabiti, mafunzo rasmi na hazikuwa na ulinzi wa haki za msingi.
Kwa nchi za Afrika Mashariki Tanzania inakuwa ni nchi ya pili baada ya Kenya kuwekeza katika mafunzo ya ujuzi na elimu ya haki kwa wafanyakazi wa nyumbani, hatua inayolenga kuwainua kutoka sekta isiyo rasmi hadi taaluma yenye hadhi na viwango.
Kwa Tanzania, juhudi za kuimarisha sekta ya kazi za ndani zimepata msukumo kupitia ushirikiano wa Serikali na wadau wa kimataifa.
Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) kwa kushirikiana na vyama vya wafanyakazi limekuwa likitoa mafunzo ya haki za wafanyakazi, ustawi kazini na misingi ya mikataba kwa watumishi wa nyumbani katika mikoa kama Mwanza na Arusha.
Pia, mafunzo hayo yanafanyika kutokana na kuongezeka kwa soko la uhitaji wa wafanyakazi wa majumbani wenye ujuzi.
Hivyo, Shirika la Watu wanaojitolea Ulimwenguni (CVM) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), wapo katika hatua za mwisho za kuandaa mtalaa wa kozi ya muda mrefu ngazi ya diploma kwa ajili ya wafanyakazi hao.
Hayo yamesemwa leo Jumatano, Februari 18, 2026 na Mkurugenzi wa CVM, Magesa Nathanael kwenye mkutano wa kuhitimisha mradi wao wa kwanza wa kuwajengea uwezo wafanyakazi hao uliokuwa ukitekelezwa kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani, Mahoteli, Huduma za Kijamii na Ushauri (Chodawu).
Nathanael amesema hatua hiyo inakuja baada ya kuona matunda kwa wafanyakazi waliopata fursa ya mafunzo ya muda mfupi katika mradi huo uliokuwa ukitekelezwa kwa miaka mitatu.
“Katika mafunzo hayo kwa kushirikiana na Veta tulifanikiwa kuandaa mtalaa wa kufundisha kazi za nyumbani, uliokuwa wa mwezi mmoja hadi sita na baada ya hapo wapo wafanyakazi walioongeza ujuzi na kubadili ufanyaji kazi wao tofauti na ilivyokuwa awali.
“Lakini, sasa tumeona kuna haja ya kuuboresha uwe ni wa kozi ndefu, mwanafunzi anaweza kukaa darasani hadi miaka miwili,” amesema.
Mkurugenzi wa Mafunzo Veta, Dk Abdallah Ngodu amesema mwanafunzi atakayesoma kozi hizo atakaa darasani miaka miwili hadi mitatu kama anataka kuwa kwenye umahiri zaidi.
“Akiwa ngazi ya tatu anaweza kuwa mahiri zaidi, kusimamia wenzake au kuendelea na elimu ya juu. Kwani mafunzo ya ufundishaji yanaruhusu mtu anapokuwa anamaliza diploma anaweza kuendelea na digrii,” amesema Dk Ngodu.
Amesema kati ya vitu atakavyovisoma mwanafunzi ni pamoja na usafi, kupika, huduma ya malezi kwa watoto na wazee, haki za kazi na ustahimilivu na ukarimu.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Majumbani, Zanini Athuman amesema hilo ni jambo zuri kwa kuwa, litasaidia kazi hiyo kuthaminika na kuheshimiwa.
Amesema fani hiyo imekuwa ikidharauliwa kwa kuwa wengi wao wametoka majumbani kwao wakiwa hawana taaluma yoyote na pia itawawezesha hata kukua na kupata ajira yenye mshahara mzuri zaidi.
“Mfano kama Veta wameanzisha mapishi ya keki, hivyo kuwaongezea kitu cha ziada wafanyakazi hawa ni kujiongezea kipato,” amesema Zanini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Rashid Ally Salim amesema Serikali zote zinatambua umuhimu wa wafanyakazi hao.
Salim amesema ndio maana hata katika kutangazwa kwa kima cha chini cha mshahara, wafanyakazi hao walihusishwa japo utekelezaji wake kwa waajiri wengine umekuwa mgumu.
Awali, akieleza kuhusu mradi huo wa kuwawezesha wafanyakazi, Mwanasheria wa Chodawu, Asteria Mathias amesema katika utekelezaji wa mradi huo jumla ya wafanyakazi 1,244 wamepata mafunzo na kuhitimu.
Mathias amesema kutokana na mafanikio ya mradi huo, utatekelezwa kwa awamu ya pili na sasa utaenda mikoa 14 badala ya tisa.
Amesema mradi huo utasaidia kuongeza taaluma, kukuza ujuzi na kuongeza kipato.
Mafunzo hayo yana manufaa ya moja kwa moja kwa mfanyakazi na Taifa ikiwamo kuinua hadhi ya kazi za ndani, kuongeza ujuzi wa kazi za nyumbani kwa viwango vya kitaalamu, kujifunza haki za mfanyakazi na usalama wa kazi.
Faida nyingine ni kujiandaa kufanya kazi ndani au nje ya nchi kwa kujiamini, kuongeza nafasi ya kupata ajira bora na mshahara wa haki.
Usafi wa kisasa hauishii kung’arisha sakafu, ni sayansi ya taratibu, vifaa na kemikali sahihi.
Mafunzo ya huduma ya usafi wa nyumba yanahimiza upangaji kazi kwa ratiba, utambuzi wa aina za nyuso (kioo, mbao, marumaru) na matumizi salama ya kemikali ili kuepusha madhara kwa afya na mali.
Aidha, kufua na kupiga pasi si shughuli za kubahatisha, ni ustadi unaohusisha kuchambua vitambaa kwa alama za lebo, kudhibiti joto la pasi na kuhifadhi mavazi kwa mpangilio unaoepusha unyevu na harufu.
Kwa familia nyingi, ubora wa usafi umeanza kuonekana kama kipimo cha hadhi na ustawi, hapo ndipo taaluma hii inapata heshima inayostahili.
Huduma za chakula nyumbani imebadilika, msaidizi wa jikoni au mpishi wa familia anatakiwa kujua si tu mapishi ya vyakula vya kawaida, bali pia misingi ya vyakula vya kimataifa kuanzia pilau, biriani hadi pasta na saladi za kisasa.
Usafi wa jikoni ni nguzo kuu, hapa, mafunzo huzingatia uhifadhi sahihi wa chakula kwa kuzingatia joto linalofaa, kutenganisha vyakula vibichi na vilivyopikwa na kuzuia uchafuzi mtambuka.
Katika malezi, mtaalamu anapaswa kuelewa hatua za ukuaji wa mtoto kimwili, kiakili na kihisia. Hii inahusisha kupanga michezo na shughuli zinazochochea ubunifu, lugha na ustadi wa kijamii.
Mafunzo ya huduma ya kwanza huwapa walezi uwezo wa kukabiliana na dharura ndogo kama kuungua au kuanguka, huku wakijua mipaka yao na wakati wa kumtaarifu mzazi au mtaalamu wa afya.
Aidha, nidhamu chanya ambayo haitegemei adhabu kali bali mazungumzo na kuelekeza, imeonekana kujenga watoto wenye kujiamini na kuwajibika.
Hii ni falsafa inayokubalika kimataifa na inayoongeza thamani ya mlezi katika soko la ajira.
Kadri jamii inavyoongezeka, mahitaji ya wahudumu wa wazee yanaongezeka. Msingi wa huduma hii ni heshima kwa utu wa mzee, uvumilivu na uelewa wa changamoto za kiafya kama shinikizo la damu, kisukari au matatizo ya kumbukumbu.
Mafunzo hulenga pia usalama wa mazingira kuepuka vitu vinavyoweza kusababisha kuanguka, kuhakikisha mwanga wa kutosha na kufuatilia matumizi ya dawa kwa usahihi. Hapa, huruma na umakini ni sifa zinazotangulia hata uzoefu.