Vijana waandaliwa kutumia fursa za kidigitali

Dar es Salaam. Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini wamejengewa uwezo juu ya namna wanavyoweza kujiandaa kikamilifu kutumia fursa za uchumi wa kidijitali kupitia programu ya Smart Elite Initiative iliyozinduliwa.

Uzinduzi wa Smart Elite Initiative umefanywa na Ofisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo, leo Jumatano, Februari 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Nshekanabo amesema kuunganisha elimu, teknolojia na ujasiriamali katika jukwaa moja linalowalenga wanafunzi wa elimu ya juu nchini kunadhihirisha utayari wa wadau katika kuwainua vijana kushiriki kuchangia maendeleo ya uchumi wa kisasa ndani ya jamii wanayotoka.

Uzinduzi huo, uliofanyika kupitia ushirikiano wa Taasisi ya CRDB Bank Foundation, umeungana na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) pia ulitumika kama njia ya kuwahamasisha wanafunzi kurejesha mikopo wanayoichukua kwa ajili ya kufanikisha ndoto zao.

“Kwa uzinduzi wa programu ya Smart Elite Initiative unaofanyika leo, tunajenga daraja linalowaunganisha wanafunzi kutoka darasani kwenda kwenye ushindani wa soko la ajira na ulimwengu wa ubunifu unaowahitaji kwa shauku kubwa. Katika dunia ya sasa, majukwaa ya kidijitali yanachangia kutoa maarifa ya kitaaluma. Vijana wanapaswa kuwa na uwezo wa kubuni na kuendesha miradi,” amesema Nshekanabo.

Kupitia ushirikiano wa taasisi hizo tatu, yaani CRDB Bank Foundation, kampuni ya Basil Link na HESLB, Nshekanabo amesema unaunda mfumo shirikishi unaojibu changamoto zinazowakabili vijana kwa vitendo.

Katika ushirikiano huo, Taasisi ya CRDB Bank Foundation itajikita katika kutoa elimu ya fedha na mafunzo ya ujasiriamali, ushauri elekezi (mentorship) pamoja na mkopo wa kompyuta mpakato kwa wanafunzi wenye uhitaji.

“Benki ya CRDB na CRDB Bank Foundation tunatambua kwamba kompyuta ni nyenzo muhimu ya kujifunzia kwa wanafunzi wa elimu ya juu, lakini si wote wanamudu bei yake sokoni, ndio maana tumejitoa kusaidia upatikanaji wake kirahisi,” amesema Nshekanabo.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema mpango wa Smart Elite Initiative unamlenga mwanafunzi yeyote wa elimu ya juu ambaye ni mnufaika wa HESLB.

Ili mwombaji anufaike na programu hiyo, atatakiwa kuwa mwanafunzi wa chuo kikuu au taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa na awe tayari kushiriki mafunzo yanayotolewa na CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na bodi ya mikopo.

“Sifa nyingine muhimu ni mwombaji kuwa na nidhamu ya fedha pamoja na utayari wa kuwajibika katika fursa atakazozipata. Tukishirikiana na kampuni ya Basil Link, CRDB Bank Foundation tutawapa kompyuta mpakato wanafunzi wote wenye uhitaji kwa makubaliano ya kulipa kidogo-kidogo,” amesema.

“Tunaamini kompyuta hizi zitawasaidia wanufaika kujifunza zaidi na kutafuta fursa zinazoweza kuwanufaisha,” amesema Tully Esther.

Mkurugenzi wa Mikopo wa HESLB, Dk Peter Mmari, amesema kwa mwanafunzi anayepokea mkopo kutoka bodi, anatakiwa kufahamu kwamba Serikali imemwamini, hivyo anatakiwa kuonesha uwajibikaji wa kurudisha ili fedha hizo ziendelee kuwanufaisha watoto wengine wa Kitanzania kupata elimu itakayowasaidia kuongeza uelewa wa mambo.

“Tunashirikiana na wadau wengine kama CRDB Bank Foundation kutoa elimu kwa wanufaika wetu ili kuhakikisha fedha zilizotolewa zinarudi.

“Ukiwa na tabia ya kukopa na kulipa, unakuwa rafiki mzuri wa taasisi za fedha, ni suala ambalo wahitimu wetu wanatakiwa kulifahamu. Ninawaomba wanufaika wote wa bodi ya mikopo kukumbuka hilo na kutimiza wajibu wa kulipa madeni waliyonayo,” amesema Dk Mmari.

Akieleza namna wanafunzi wanavyoweza kunufaika na Programu ya Smart Elite Initiative, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Basil Link, Emmanuel Basil, amesema wanaowawakilisha katika vyuo vikuu vingi nchini watakuwa wanatoa ufafanuzi kwa mwanafunzi yeyote mwenye swali.

“Katika utekelezaji wa mpango huu, Smart Elite Initiative, tunataka kuona mwanafunzi wa Kitanzania anahitimu chuo kikuu akiwa na cheti pamoja na ujuzi wa vitendo, maono ya kibiashara na nidhamu ya fedha,” amesema.

“Mimi ni miongoni mwa wanufaika wa Programu ya IMBEJU, ambaye nilianza kushiriki mafunzo yanayotolewa tangu nikiwa chuo, ninaamini wanafunzi wanaoendelea vyuoni wanaweza kunufaika kama ilivyokuwa kwangu,” amesema Basil.