UPAMBANAJI wa kiungo Mtanzania, Zuwena Aziz ‘Zizou’ anayechezea timu ya Mogbwemo Queens inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Sierra Leone, haukuwa rahisi kuna kipindi alitamani kuachana kabisa na mchezo huo wa soka.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, anasimulia mwaka 2017 akiwa Baobab Queens iliyomsajili kutoka Thika ya Ligi Kuu Kenya, hakuwahi kupata pesa yoyote, kitu ambacho kilimvunja moyo na kuona anafanya kazi bure.
“Nilipigiwa simu na viongozi wa Baobab nirudi Tanzania kuisaidia timu isishuke daraja, nikawapelekea na wachezaji wawili Easter na Kamalu kutoka Thika sambamba na kipa wa timu ya taifa ya Uganda, Judith, tuliishi maisha magumu sana hadi tukawa tunakwenda kuomba kucheza ndondo mtaani ili tupate pesa ya kujikimu kama wanawake,” anasema ‘Zizou’ akifafanua jina lake la utani lilitokana na kumkubali mchezaji wa zamani na kocha wa Real Madrid, Zinedine Yazid Zidane maarufu kama ‘Zizou’.
Anasema japo soka la wanawake halina thamani kama lile la wanaume, kinachomsukuma aendelee mbele ni ndoto zake za kuhakikisha anaikomboa familia yake kiuchumi.
“Mimi ni mzaliwa wa tatu kati ya watoto watano, mmoja yupo serikalini, mwingine chuo na wengine wapo tu, napambana ili niwe msaada kwa wazazi wangu na yapo mambo niliyoyafanya angalau kidogo wamekula jasho langu,” anasema Zizou.
ZUWE 06
Anasema maisha ya Sierra Leone yana changamoto hasa katika suala la chakula ambako wanapenda kupika ubwabwa wa kuchemsha, kisamvu wanachochanganya na samaki na kuweka pilipili nyingi wanazofanya kama nyanya.
“Pia hawana ukarimu kama ilivyo Tanzania. Kila mtu ana mambo yake, lakini kitu cha tofauti mashabiki wanajaa uwanjani kuangalia mechi za wanawake,” anasema mwanadada huyo.
Anasema hatasahau changamoto aliyopata Morocco wakati anaichezea klabu ya Nahaj Souss, hawakuwa wakimpa mshahara na baada ya kumaliza mkataba na muda wa viza ukawa umeisha, hivyo wakawa wanataka kutumia kama fimbo ya kumuumiza.
“Nilikuwa na rafiki yangu polisi, raia wa Morocco, aliniambia niende mahakamani ili nipate viza, lakini nilisaidiwa sana na Balozi wa Tanzania aliyekuwa nchini humo, nikafanikiwa na walinipa pesa zangu zote, ambazo zijazitumia hadi sasa, nikirudi Tanzania nawaza kufanya kitu kikubwa cha kumbukumbu,” anasema Zizou anayemiliki kituo cha kufanisha mazoezi (gym) inayoitwa Zizou, ikiwa ni moja ya jasho la kuutumikia mipira wa miguu.
Timu alizozichezea ni Kigoma Sisters, Baobab Queens, Uzuri Queens, Evergreen Queens, Ceasiaa Queens, Tausi FC, Thika Queens ya Kenya, Lady Doves FC ya Uganda, Nahaj Souss ya Morocco na sasa Mogbwemo Queens inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Sierra Leone.
UGUMU WA KUANZISHA FAMILIA
Anasema ingawa sio kwa wote, ila miongoni mwa sababu zinazowakwamisha kuanzisha familia ni kutokuwa tayari kumilikiwa na wanaume, muonekano na kukosa hisia zinazomalizwa kwa kufanya mazoezi magumu.
“Wachezaji wengi hatupo tayari kutawaliwa, mfano unapoolewa lazima utatakiwa kumsikiliza mumeo anachotaka, wakati huo huo unataka kufanya mazoezi na kukaa kambini, sasa inakuwa ngumu muda anaokuwa anakuhitaji unakuwa na ratiba nyingine,” anasema Zizou na kuongeza:
“Wapo baadhi ya wanaume wakiona mavazi tunayovaa wanakuchukulia kama ni mshikaji wao, nimewahi kupata changamoto wakati napita mtaani, watu walikuwa wanajiuliza kama mimi ni mwanaume au mwanamke, lakini nilichukulia poa, kwani siwezi kubadilisha kitu kwani nimezoea.”
Anaulizwa kuna uhusiano gani kati ya soka na wanawake kuvaa nguo za kiume? Anajibu: “Ni mazoea na pia mwili unakuwa umejengeka kimazoezi, hivyo ukivaa nguo za kike unakuwa kama unachekesha.”
ANATAKA WATOTO, SIO KUOLEWA
Anasema baada ya Ligi kumalizika, akirejea Tanzania anatamani kuzaa na endapo Mungu akimjaalia mtoto wa kiume, lakini suala la kuolewa anajiona hayupo tayari kwa sasa.
“Nataka kuzaa mtoto mmoja tu, nina mtu wangu ni msanii, nilikutana naye uwanjani tukapendana, hivyo anajua ninataka kuzaa sio kuolewa, kwani najiona sipo tayari kufanya majukumu ya mke kwa sasa,” anasema.
Je, kutokana na kufanya mazoezi kwa nguvu kunakufanya usiwe romantiki? Anajibu: “Nikipenda mimi ni romantiki sana, mambo ya mpira nayapa muda wake na mapenzi muda wake.”
Anasema kabati lake limejaa nguo za kiume ambazo anavaa mara nyingi, lakini inapofika mfungo wa Ramadhani, anapoenda kuswali anavaa dera, akimaliza anavua na kuvaa nguo za kiume.
“Kuhusu meza yangu ya vipodozi, inakuwa na mafuta ya mchanganyiko pamoja na manukato pia nikiwa nyumbani napika mfano tambi, kutengeneza bustani, kufua na kuosha vyombo,” anasema mwanadada huyo.