Bakari Mahundu
February 24, 2026
0 Comments
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vya kihalifu ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, akisisitiza kuwa operesheni zinaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 24, 2026, Muliro amesema katika operesheni za hivi karibuni, jeshi hilo limefanikiwa kukamata simu zaidi ya 108 pamoja na vyombo vya moto, ambavyo vinadaiwa kutumika katika matukio mbalimbali ya uhalifu. Aidha, watuhumiwa kadhaa wamekamatwa kuhusiana na matukio hayo na hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao.
Kamanda Muliro ameeleza kuwa baadhi ya wahalifu wamekuwa wakitumia vyombo vya moto kutekeleza uhalifu wa uporaji na wizi, hali inayohatarisha usalama wa wananchi. Hata hivyo, amesema Jeshi la Polisi limejipanga kukabiliana na vitendo hivyo kwa kuongeza doria na operesheni za kushtukiza katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu au watu wanaotiliwa shaka, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya polisi na jamii ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu.
“Hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kihalifu. Lengo letu ni kuhakikisha Dar es Salaam inabaki kuwa salama kwa wote,” amesema Muliro.
SACP Jumanne Muliro amesema maneno ya mitandaoni yanayozungumzwa kumhusu ZCO, SACP Faustine Mafwele ni kama Riwaya za Kufikirika.
Muliro ameyasema hayo wakati akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua ukweli kuhusu mahali alipo Mafwele.