Mwanza. Wakati ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha tano kutoka Isaka mkoani Shinyanga hadi Fela mkoani Mwanza ukifikia zaidi ya asilimia 68, wakazi wa mikoa hiyo wametakiwa kuchangamkia fursa za kiuchumi zitakazotokana na mradi huo wa kimkakati.
Akizungumza leo Jumanne Februari 24, 2025 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha reli hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango vya kimataifa, hivyo ni wajibu wa wananchi kujiandaa kunufaika na miundombinu hiyo.
Profesa Mbarawa amesema kipande hicho chenye urefu wa kilomita 341 kinajengwa kwa gharama ya dola za Marekani bilioni 1.326, sawa na zaidi ya Sh3.06 trilioni na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na China Railway Construction Corporation (CRCC), ambapo kitakamilika 2028 baada ya ujenzi wake kuanza 2021.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa reli ya kisasa eneo la Fela Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. Picha na Saada Amir
“Nimekuja leo kutembelea mradi wetu wa SGR kipande hiki cha kutoka Isaka hadi Mwanza. Tumeanzia Mwanza tukaona kazi inaendelea vizuri na sasa tuko hapa Fela, eneo hili ni muhimu kwa sababu hapa ndipo patakapokuwa kituo kikuu cha kubadilishia mizigo, kubadilishia treni na kufanya matengenezo,” amesema.
Ameeleza kuwa kituo hicho kitakuwa miongoni mwa vituo vikuu vitatu nchini, vingine vikiwa Kwara (Tabora) na Uvinza ambako kuna reli inayounganisha Kigoma na Burundi na kuwa Fela itakuwa kitovu cha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Kanda ya Ziwa na nchi jirani.
“Nawaomba sana wananchi wajipange kuchangamkia fursa hizi…kutakuwa na shughuli nyingi na kubwa zitakazotoa ajira na kipato kwa watu wa hapa. Lakini pia tuwe walinzi wa mali za mradi, ukichukua saruji au mafuta umeiba mali ya Watanzania,”amesisitiza.
Meneja Mradi wa Kipande cha ujenzi wa reli ya kisasa cha Isaka-Mwanza, Morgan Masunga akitoa maelezo ya mradi kwa Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alipokuwa kwenye ziara ya kuukagua. Picha na Saada Amir
Kwa upande wake, Mbunge wa Misungwi, Silvery Luboja amesema wananchi wa wilaya hiyo wanashukuru kwa miradi mikubwa inayotekelezwa katika eneo lao na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla ikiwemo SGR, daraja la Busisi na meli ya MV Mwanza.
Amesema miradi hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea Watanzania maendeleo yenye tabasamu la utu ambayo wataitumia kwa ajili ya kusafirisha bidhaa zao kibiashara na kukuza uchumi wao na wa Taifa.
“Nakumbuka Mheshimiwa Rais wakati anazindua Bunge la 12 alisema atawaachia Watanzania tabasamu la utu katika awamu ya sita…mimi naona tayari tabasamu hilo lipo Misungwi. Ukiangalia daraja la JPM, Meli ya Mv New Mwanza na huu mradi wa SGR ni fursa kubwa kwetu,”amesema.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa reli ya kisasa eneo la Fela Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. Picha na Saada Amir
Luboja ametoa wito kwa wananchi kutumia miundombinu hiyo kujinufaisha kiuchumi kwa kusafirisha mazao na bidhaa za biashara kwenda masoko ya ndani na nje ya nchi na kuwahamasisha wawekezaji kuangalia fursa katika kata za Fela na Usagara, ambako kunatarajiwa kuwa na bandari kavu (ICD) na stesheni kuu ya abiria.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la reli Tanzania (TRC), Machibya Masanja ameiomba Wilaya ya Misungwi kupangilia vizuri eneo la Fela kwa matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro na fidia kubwa baadaye kwa Serikali.
Amesema bila maandalizi mazuri, eneo hilo linaweza kuvamiwa na makazi holela na kuigharimu Serikali fedha nyingi za fidia.
Ameongeza kuwa TRC itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha miundombinu ya kuhudumia mizigo, huku lengo likiwa ni ifikapo mwaka 2028 treni ziwe na uwezo wa kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa ufanisi.