Mtoto wa Mjini – 6

HUKU akiendelea kuwatazama kwa zamu vijana wale kutaka kuwakumbuka kama aliwahi kuwaona mahali, mzee Mangushi alijibu: “Marhaba…”
Na baada ya kutambua sura zao zilikuwa ngeni machoni pake, akawauliza: “Niwasaidie nini?”
 “Kuna shida kidogo mzee wangu,” alisema mmoja wao na kumfanya mzee Mangushi kuutoa mwili wake wote nje ya mlango.
“Shida gani tena?” alihoji uso wake ukitaliwa na wasiwasi.
“Mimi ni Inspekta Haroub na mwenzangu ni Sajenti Chris,” walijitambulisha huku kila mmoja akitoa kitambulisho chake na kumuonyesha mzee Mangushi. 
Mzee Mangushi aliviangalia vitambulisho kwa umakini mkubwa na kuwaangalia vijana wale na kuthibisha sura zao zilikuwa zikirandana na zile zilizokuwapo kwenye vitambulisho vyao.
Mzee Mangushi alipatwa na mshtuko na kujiuliza sababu za maaskari wale kufika nyumbani kwake lakini hakutaka kuuonyesha, akakumbwa na ushawishi zaidi wa kutaka kujua sababu zaidi ya kufika nyumbani kwake.
“Unamiliki gari aina ya Toyota IST?” Inspekta Haroub alimuuliza na akazitaja namba za gari hiyo.
“Ndio ni gari yangu…” Swali hili lilimfanya mzee Mangushi kupitisha kwa haraka baadhi ya mambo kichwani mwake akifikiria kama gari yake ilikuwa imeibwa au imepata ajali.
“Iko wapi?”Inspekta Haroub alimuuliza.
“Anayo kijana wangu, ndiye anayeiendesha kama teksi…”
“Ni mwanao au…?”
“Naweza kusema ni mwanangu lakini sio wa kumzaa…”
“Unaishi naye hapa nyumbani?”
“Hapana, ni kijana wa jirani yangu…”
“Tunaweza kumpata…?”
“Bila ya shaka… anaishi jirani tu hapa…” alisema mzee Mangushi huku maswali yakizidi kumtembea kichwani mwake kutaka kujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea.
“Hamuwezi kunidokeza japo kidogo kilichotokea?” alihoji mzee Mangushi.
“Ingekuwa vizuri tungezungumza naye nawe ukiwapo…” Inspekta Haroub alimwambia. 
Ilimbidi mzee Mangushi kuwaomba maaskari wale arudi ndani na kumdokeza mkewe kuhusu ujio wao na kumtaka asitishe kumtengea kahawa yake.
“Shida ni nini?” Bi Swabra alitaka kujua.
“Sijui, maana hawajanidokeza chochote, ngoja niende nao, nikirudi nitakueleza kwa kina.”
“Ungekunywa kahawa kwanza…polisi hawana dogo.” 
“Ngoja niwapeleke kwa mzee Manyara kwanza, nitakuja kunywa nikirudi…” 
“Sawa…” alijibu Bi. Swabra huku naye akimsindikiza mumewe na akawashuhudia kweli vijana wawili waliokuwa kwenye mwonekano wa kipolisi. 

********
WAKAZI wa Kongowe waliliona gari likiwa limeegeshwa katika moja kati ya mashamba ya mtu wanayemfahamu katika kitongoji chao. 
Siku ya kwanza wengi hawakuwa na wasiwasi na gari hilo, walidhani lilikuwa likifahamika na mwenye shamba, baadhi walifikiria labda kulikuwa na uhusiano kati ya mwenye gari na mwenye shamba.
Ilidhaniwa mwenye shamba alikuwa amepata mgeni kutoka mjini aliyefika kumsalimia na kuamua kuliegesha gari lake pale kwa muda wakati wakienda nyumbani kuzungumza, wakalipuuza na kuendelea na shughuli zao.
Lakini kadiri muda ulivyokuwa ukisonga, ndivyo wasiwasi ukaanza kuwaingia baadhi yao na kujiuliza kutokana na kuliona gari lile likiwa limeegeshwa pale kwa muda mrefu.
Jioni ilipoingia na gari lile liliendelea kuwapo palepale, wasiwasi ukazidi. 
Siku ikaisha, asubuhi kulipopambazuka bado gari lilikuwepo palepale, ndipo baadhi ya wananchi walipoingiwa na wasiwasi, wakaanza kulitilia shaka uwepo wa gari lile katika eneo lao.
Wakahoji kuhusu uwepo wa gari lile, habari zikamfikia mwenye shamba ambaye naye alikana kulifahamu na kueleza kwamba hakuwa amempokea mgeni yeyote mwenye kulimiliki gari lile.
Taarifa zikatolewa kwa mjumbe wa kitongoji ambaye naye akazifikisha Serikali ya Mtaa. Polisi walipewa taarifa kuhusu uwepo wa gari lile na mwenyekiti wa serikali ya mtaa. 
Polisi walipofika na kulikagua, wakahisi ndilo gari lililohusika katika tukio la uhalifu lililofanyika Dar es Salaam.
Ni kwa sababu tayari walikuwa na taarifa za wizi uliotokea na kuhusisha gari aina hiyo kupitia mtandao wa jeshi la polisi.
Taarifa ya kuonekana kwa gari hilo zikafikishwa jijini Dar es Salaam na hatimaye zikafika katika kituo cha Polisi cha Msimbazi ambako tukio hili lilikuwa limeripotiwa.
Askari wa upelelezi kutoka katika kituo hicho, Inspekta Haroub na Sajenti Chris walifika Kongowe na kulikagua gari hilo na kujiridhisha kwamba ndilo lililohusika katika tukio la kuibiwa kwa Kamba Makambo.
Askari hao waliongozana na wenzao wa Pwani ambao nao walifika eneo la tukio wakiwa kama wenyeji wa eneo hilo kiusalama.
Katika uchunguzi ilibainika hakukuwa na kitu chochote kilichokuwa kimeibiwa ndani ya gari na lilikuwa na mafuta ya kutosha kuweza kulifikisha Dar es Salaam. Aidha, waliukuta ufunguo wa gari ukiwa imechomekwa katika sehemu yake ukining’inia. 
Walipomaliza kufanya ukaguzi wao, walilichukua hadi katika kituo kikuu cha Polisi kilichopo Kibaha na kuandikisha maelezo, kisha Inspekta Haroub na Sajenti Chris waliliendesha kurudi nalo Dar es Salaam. 

*********
MZEE Tuesday Manyara alikuwa akipata kifungua kinywa wakati rafiki yake wa muda mrefu, mzee Mangushi alipowasili na watu wengine wawili nyumbani kwake.
“Hodiii…” alibisha mzee Mangushi.
“Karibu mpaka ndani…” alitikia mzee Manyara aliyekuwa ameketi katika kiti kilichokuwapo kwenye ukumbi wa nyumba hiyo baada ya kuigundua sauti ya swahiba yake.
“Asante… habari za hapa…?”
“Nzuri… karibuni.”
Mzee Manyara alipowaona wageni wengine waliofuatana na swahiba yake, akaomba kuongezewa viti vingine.
Baada ya kuketi mzee Manyara akawakaribisha wageni wake chai, lakini wakashukuru na kudai wameshakunywa.
“Hawa bwana ni wageni wetu…” alianza kusema mzee Mangushi akimfahamisha jirani yake na kuwataka wanausalama wale kujitambulisha wenyewe na kueleza shida yao. 
“Karibuni…” mzee Manyara aliwakaribisha huku akiwangalia kwa zamu.
Ilikuwa ni zamu ya Inspekta Haroub na Sajenti Chris kujitambulisha kwa mzee Manyara.
“Shida yetu kubwa tunamhitaji mwanao.. Muddy… ambaye anayeendesha gari ya bwana Mangushi…” alisema Inspekta Haroub baada ya kujitambulisha.
“Muddy…!” alisema mzee Manyara ilhali akionyesha kuwa na wasiwasi kama mwanaye huyo alikuwapo chumbani kwake.
“Huyu bwana utaratibu wake wala haueleweki, unaweza kukuta yupo ndani amelala au wakati mwingine anakuwa kwenye kazi yake hiyo…” alisema mzee Manyara.
“Hebu aangaliwe ndani…” alisema Inspekta Haroub.
Mzee Manyara aliinuka na kwenda kugonga chumba cha Muddy akifuatana na Inspekta Haroub na Sajenti Chris.
Waligonga mlango lakini hawakuitikiwa na walipousukuma mlango ulifunguka, wakaingia ndani lakini hakukuwa na dalili ya kuwepo kwa Muddy.
“Mara ya mwisho ulimuona lini?”
“Kwakweli mimi sijaonana naye kwa muda mrefu…inaweza kufika hata wiki labda mama yake…”
Bi Faudhia aliitwa na kuulizwa kuhusu kumuona mwanaye, naye alisema kwa mara ya mwisho alimuona siku mbili zilizopita.
“Alirudi hapa akiwa na haraka wala hakutulia kisha akaondoka na tangu siku ile sijamuona tena….”
“Anamiliki simu?” Inspekta Haroub aliuliza.
“Ndio…” alijibu mzee Manyara ambaye alimwambia mkewe aitaje namba yake kwa kuwa yeye hakuwa ameikariri kichwani mwake.
Mama yake naye alimwita dada yake Muddy aitwaye Maisha ambaye ndiye aliyeitoa namba hiyo, lakini ilipopigwa haikuwa ikipatikana.
Inspekta Haroub aliwaambia wazazi wa Muddy pamoja na mzee Mangushi walipaswa kwenda kituoni ili kuandikisha maelezo.
“Kwani shida kubwa ni nini?” aliuliza mzee Manyara.
“Mkifika kituoni mtafahamu kila kitu kinachoendelea…” alijibu Inspekta Haroub na kuwaambia hakukuwa na muda wa kuchelewa, walipaswa kuondoka muda huohuo.
“Kwani hatuwezi kuyazungumza hapa yakaisha?” alihoji mzee Mangushi.
“Haya mambo sio madogo kama mnavyofikiria lazima mfike kituoni…” alisisitiza Inspekta Haroub.
Kwa shingo upande wazee wale walikubali kufuatana na maaskari wale huku shaka zikiwatawala katika nafsi zao.     

KUTOKA Gerezani, mzee Mangushi alikodi teksi iliyowachukua watu wanne, mzee Manyara, Bi Faudhia, Sajenti Chris na yeye mwenyewe.
Inspekta Haroub aliendesha gari waliyokuja nayo huku akiwapakiza watoto wa mzee Manyara ambao ni Mina, Maisha, Meja na Kizanda.
Njiani wazazi wa Muddy na mzee Mangushi pamoja na kina Meja, Kizanda, Makisha na Mina walikuwa na wasiwasi labda Muddy alikuwa amepata ajali mbaya na kufariki dunia.
“Lakini mbona walijaribu kumpigia simu…?” Maisha alijiuliza. 
Walipofika kituoni walishangaa kuliona gari la mzee Mangushi ambalo ndilo alilokuwa akiliendesha Muddy likiwa limeegeshwa pembeni mwa kituo hicho.
Kidogo wasiwasi wa kwamba Muddy alikuwa amepata ajali mbaya na kupoteza maisha uliwatoka baada ya kuiona gari likiwa zima na halikuwa na dalili yoyote ya kupata ajali.
“Sasa shida ni nini?” Mawazo mengine yakaanza kuzitawala fikra zao na kuhisi labda Muddy alikuwa ametekwa na kuuawa ila gari lilipatikana likiwa salama.