Dar es Salaam. Benki ya Stanbic Tanzania imezindua huduma ya malipo kwa wateja wake, hatua inayolenga kurahisisha miamala ya kidijitali kwa kuruhusu malipo kufanyika moja kwa moja kupitia Stanbic App au kwa kutumia huduma ya USSD.
Uzinduzi huo unakuja baada ya mfumo wa Lipa Simpo kuwapo kwa muda, ukitumika zaidi kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali kupokea malipo kwa kutumia QR Code kutoka kwa wateja wanaotumia benki au mitandao mbalimbali ya simu nchini.
Kupitia huduma hiyo mpya, wateja wanaweza kulipia bidhaa na huduma kwa haraka na kwa usalama moja kwa moja kutoka kwenye akaunti zao za benki. bila kutumia fedha taslimu au kuhitaji chenji.
Hatua inayotarajiwa kuongeza matumizi ya malipo ya kidijitali katika shughuli za kila siku za kiuchumi.
Akizungumza jana katika eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam wakati wa ziara maalumu ya kutoa elimu kwa wateja kuhusu huduma hiyo, Mkuu wa Huduma za Kidijitali wa Stanbic Bank, Edward Balandya, amesema benki hiyo imeweka vivutio maalumu ili kuhamasisha matumizi ya mfumo huo.
Meneja wa Mawasiliano wa Benki ya Stanbic, Dickson Senzi (kushoto), na Meneja wa Kidijitali na Biashara Mtandaoni wa benki hiyo, Godlisten Shirima (kulia), wakimuonyesha Malipula Suti (katikati) jinsi ya kupokea malipo kupitia Lipa Simpo wakati wa ziara ya kutembelea maduka yanayotumia huduma hiyo jijini Dar es salaam.
Amesema katika kipindi maalumu kitakachoendelea hadi Aprili 2026, miamala yenye thamani ya zaidi ya Sh40,000 itatozwa ada ya Sh1,000 pekee, hatua inayolenga kuwahamasisha wateja kufanya malipo ya viwango vikubwa kwa gharama nafuu.
“Tunawahimiza wateja wetu kupakua Stanbic App na kuanza kutumia Lipa Simpo ili kufurahia urahisi wa kufanya malipo, salama na kwa gharama nafuu,” amesema Balandya.
Balandya ameongeza kuwa benki hiyo imeanza kampeni za uhamasishaji katika maeneo yenye shughuli nyingi za kibiashara jijini Dar es Salaam na katika miji mingine nchini, zikilenga kuwaonyesha wateja na wafanyabiashara namna ya kutumia huduma hiyo kwa vitendo.
Kampeni hizo pia zinalenga kukusanya maoni ya wateja na wafanyabiashara ili kuboresha zaidi huduma hiyo na kuhakikisha inakidhi mahitaji ya soko.
Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano wa Stanbic Bank Tanzania, Dickson Senzi amesema kuongezeka kwa matumizi ya malipo yasiyotumia fedha taslimu linasaidia kuimarisha uwazi wa kifedha pamoja na kupunguza hatari za upotevu wa fedha.
Alisema hatua hiyo pia inasaidia biashara ndogo na za kati (SMEs) kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za kifedha, jambo linalochangia kukuza biashara na uchumi kwa ujumla.
“Kampeni zetu si za maonyesho tu, bali ni utekelezaji wa vitendo unaoonesha jinsi malipo ya kidijitali yanavyoweza kufanya kazi katika maisha ya kila siku ya kiuchumi, kuanzia manunuzi ya rejareja hadi miamala ya biashara,” alisema Senzi.
Aliongeza kuwa maendeleo ya teknolojia yamefanya huduma za kifedha kupatikana kwa urahisi zaidi, hivyo ni jukumu la taasisi za fedha kuhakikisha zinatoa suluhisho salama, nafuu na zinazoaminika kwa wateja.