Serikali kupitia Wizara ya Afya imeziagiza Hospitali za Rufaa za Mikoa, Taifa, Wilaya pamoja na Vituo vya Afya kote nchini kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa na magonjwa mengine ya mlipuko, kama sehemu ya kuimarisha ulinzi wa afya ya umma.
Akizungumza Februari 25, 2026 mkoani Morogoro, Grace Magembe amesema kuwa serikali inaendelea kuviwezesha vituo vingi zaidi vinavyofanya ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa (Sentinel Surveillance Centers), hasa katika ukusanyaji wa sampuli mapema na kuziwasilisha kwa wakati katika Maabara ya Taifa.
“Kazi hii ni ulinzi wa nchi dhidi ya magonjwa ya mlipuko na hakuna mbadala,” amesisitiza Dkt. Magembe.
Onyo Dhidi ya Matumizi Holela ya Antibiotiki
Katika hotuba yake, Dkt. Magembe ameonya juu ya matumizi holela ya dawa za antibiotiki bila ushauri wa kitaalamu, akieleza kuwa tabia hiyo inachangia kuongezeka kwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa (antimicrobial resistance).

Amefafanua kuwa baadhi ya wananchi hukimbilia kununua antibiotiki pindi wanapopata dalili kama mafua, kikohozi, homa, maumivu ya kichwa au uchovu wa mwili bila kupimwa.
“Ukihisi unaumwa, nenda kwenye kituo cha tiba upimwe kwanza ujue unaumwa nini, badala ya kunywa dawa kiholela,” ameonya.
Licha ya kutangazwa kuisha kwa mlipuko wa Kipindupindu, Mganga Mkuu huyo ameutaka umma kuendelea kuchukua tahadhari za msingi za kujikinga, ikiwemo:
Hatua hizo ni muhimu katika kuzuia kurejea kwa magonjwa ya mlipuko katika jamii.
Dkt. Magembe pia amewashukuru wadau wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko, wakiwemo World Health Organization (WHO) na PATH.
Kwa upande wake, Dkt. Vida Mmbaga, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Mlipuko kutoka Wizara ya Afya, amesema Tanzania imejenga uwezo mkubwa wa kitaalamu na miundombinu katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hatua inayoiweka nchi katika nafasi nzuri ya kuimarisha usalama wa afya ya umma.