Dar es Salaam. Kuuawa kwa msemaji wa kundi la waasi la M23, Willy Ngoma, kunatajwa kuwa mwanzo wa kutetereka kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano yanayoongozwa na Qatar, ikiwa ni jitihada za kusaka amani ya kudumu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ngoma ameuawa katika shambulizi la ndege zisizo na rubani mashariki mwa DRC Jumanne, Februari 24, 2026, maofisa wawili wakuu wa waasi, mwanadiplomasia wa kikanda na mshauri wa serikali wamethibitisha.
Shambulio hilo limetokea karibu na Rubaya, Kivu Kaskazini, saa 3 asubuhi, na limekuja baada ya siku kadhaa za mashambulizi ya muda mrefu ya ndege zisizo na rubani kwenye eneo hilo, likitekelezwa na jeshi la Serikali ya DRC (FARDC), mmoja wa maofisa wakuu wa M23 ameiambia Reuters.
Rubaya ni kitovu cha kimkakati cha uchimbaji madini ya coltan kinachozalisha karibu asilimia 15 ya hazina inayosambazwa duniani, na kuifanya kuwa ngome kuu ya kifedha kwa waasi wa M23.
Hivi karibuni, serikali ya DRC imeliongeza eneo hilo kwenye orodha ya maeneo yenye rasilimali za kimkakati za uchimbaji madini zinazotolewa kwa Marekani chini ya mfumo wa ushirikiano wa madini.
Vyanzo vya mashirika ya kiraia vimeripoti mapigano makali katika maeneo kadhaa karibu na Rubaya tangu Jumapili, na kulazimisha mamia ya familia kukimbia eneo hilo.
Mauaji ya Ngoma yametokea wakati juhudi za upatanishi wa Qatar zikiendelea, ambapo Serikali ya DRC na M23 wametia saini makubaliano mjini Doha, Qatar, ya kuanzisha utaratibu wa pamoja wa ufuatiliaji na uhakiki wa usitishaji mapigano unaohusisha Qatar, Marekani na Umoja wa Afrika (AU) kama waangalizi.
Ngoma aliwekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya (EU) tangu Desemba 2022 kwa nafasi yake kama msemaji wa M23.
M23, ambayo Umoja wa Mataifa unasema inaungwa mkono na Rwanda, inadhibiti maeneo makubwa ya majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini baada ya mashambulizi ya haraka mwaka jana, na waasi waliteka miji ya kimkakati ya Goma na Bukavu.
Waasi waliuteka kwa muda mji wa Uvira Desemba 2025, na FARDC kuurudisha tena mikononi mwa serikali mwezi uliopita. DRC ilifungua tena mpaka wake na Burundi huko siku ya Jumatatu.
Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo ulituma timu ya pamoja ya wachunguzi huko Uvira wiki hii, ili kusaidia utekelezaji wa utaratibu wa ufuatiliaji wa usitishaji mapigano uliokubaliwa mjini Doha na kutathmini hali ya usalama katika eneo hilo.
Novemba 16, 2025, waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda na Serikali ya DRC walisaini makubaliano ya mpango wa amani mashariki mwa nchi hiyo.
Hafla hiyo ilifanyika Qatar, na nchi hiyo pamoja na Marekani na Umoja wa Afrika wamekuwa wakijaribu kupatanisha kukomesha miongo kadhaa ya migogoro katika eneo hilo lenye rasilimali nyingi.
Mauaji ya Ngoma yamejiri wakati juhudi za kusaka amani zinazoongozwa na Qatar zikiendelea, ambapo DRC na M23 zilisaini makubaliano ya pamoja ya kuanzishwa kwa kikosi cha uangalizi wa usitishaji vita.
Kikosi hicho kitajumuisha, pia, waangalizi kutoka Qatar, Marekani na Umoja wa Afrika ili kuhakikisha kwamba makubaliano hayo yanafikiwa.
Hata hivyo, wakati mchakato huo haujakamilika, tayari msemaji wa M23 ameuawa, jambo linaloibua wasiwasi wa kuendelea kwa mchakato wa usitishaji vita katika eneo hilo la Mashariki mwa DRC kama walivyokubaliana.
Mwaka jana, M23 iliteka miji mikuu ya eneo la mashariki mwa DRC ya Goma na Bukavu. Majaribio ya awali ya kupata amani yalishindikana, jambo lililozisukuma nchi nyingine kuingia kati kutafuta.
Serikali ya DRC inataka kuondolewa kwa wanajeshi wa Rwanda kutoka eneo lake. Rwanda nayo imesema hilo linaweza kutokea waasi wa FDLR wenye makazi yao DRC watakaposambaratishwa.
Kundi la FDLR, kwa kiasi kikubwa, linaundwa na Wahutu wanaodaiwa kuhusika katika mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.
Juni 2025, mazungumzo kati ya Rwanda na DR Congo yaliyosimamiwa na Marekani yalisababisha kusainiwa kwa makubaliano ya amani, ambayo yalipongezwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, kama “ushindi,” lakini yalikiukwa haraka na pande zinazopigana.
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Innocent Shoo, amesema kuuawa kwa Ngoma, mmoja wa watu muhimu ndani ya M23, kunakuja katika wakati nyeti ambapo juhudi za upatanishi zinazoongozwa na Qatar zimekuwa zikijaribu kurejesha mazungumzo yao.
Amesema tukio hilo linaweza kutazamwa kama mafanikio ya kijeshi kwa upande mmoja, lakini kisiasa linafungua maswali mazito kuhusu mustakabali wa mchakato wa amani katika ukanda huo.
“Kihistoria, kuuawa kwa kiongozi wa kundi la waasi hakumaanishi mwisho wa mgogoro, mara nyingi hubadilisha tu sura yake. Ndani ya M23, kifo cha Ngoma kinaweza kusababisha ama kuibuka kwa uongozi mpya wenye mtazamo wa mazungumzo, au mgawanyiko wa ndani unaoweza kuzalisha makundi madogo yenye misimamo mikali zaidi.
“Ikiwa alikuwa miongoni mwa sauti zenye msimamo mkali, kuuawa kwake kunaweza kutoa dirisha la kimkakati kwa wapatanishi wa Qatar kusukuma ajenda ya maridhiano kwa kasi zaidi,” amesema Shoo.
Hata hivyo, amesema kama tukio hilo litatumiwa kama kichocheo cha kulipiza kisasi au kuimarisha propaganda za kivita, linaweza kuchelewesha au hata kudhoofisha mazungumzo yaliyokuwa yakijengwa kwa uangalifu.
Athari zake, pia, amesema zitapimwa kwa namna serikali ya DRC itakavyolitafsiri. Iwapo itachukulia kuuawa kwake kama ushindi wa kijeshi unaopunguza uhitaji wa maafikiano ya kisiasa, basi mchakato wa amani unaweza kupoteza kasi.
Lakini kama pande zote zitatambua kuwa mgogoro wa Mashariki mwa DRC una mizizi ya kina, ikiwemo ushindani wa rasilimali, siasa za kikabila na mvutano wa kikanda, basi tukio hilo linaweza kuwa kichocheo cha kutafakari upya umuhimu wa suluhisho la kudumu badala ya ushindi wa muda mfupi.
“Hili ni tukio la kimkakati la muda mfupi, si mabadiliko ya kimuundo. Amani ya kudumu haitatokana na kuuawa kwa mtu mmoja, bali na dhamira ya kisiasa, ushirikiano wa kikanda, na utekelezaji wa makubaliano yatakayohakikisha usalama na ushirikishwaji wa jamii za eneo hilo,” amesema.
Shoo amesisitiza kwamba swali kuu sasa si nani ameuawa, bali kama mazingira ya mazungumzo yataimarishwa au yatatikisika zaidi.
“Kuuawa kwa Willy Ngoma kunaweza kuwa ama dirisha la fursa au chanzo cha mkwamo mpya, majibu yake yatategemea si tukio lenyewe, bali uamuzi wa kisiasa utakaofuatia,” amesema.