Bakari Mahundu
February 25, 2026
0 Comments
Watu watatu ambao majina yao bado hayajatambuliwa wamefariki dunia kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha magari mawili ya mizigo yaliyogongana uso kwa uso na kuteketea kwa moto katika barabara kuu ya Morogoro–Dar es Salaam.
Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia Februari 25, 2026, katika eneo la Maseyu, Kata ya Gwata, Wilaya ya Morogoro, ambapo madereva wa magari yote mawili pamoja na mtu mmoja aliyekuwa ndani ya gari lililobeba mafuta walipoteza maisha papo hapo.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari lililokuwa limebeba mbao, aliyeshindwa kuzingatia njia yake na kuingia upande wa gari lililokuwa limebeba mafuta, hali iliyosababisha mgongano huo na kusababisha moto mkubwa.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Sajenti Pius Lugano, amesema walipokea taarifa za tukio hilo majira ya saa nane usiku, na kufika eneo la ajali kwa haraka, ambapo walifanikiwa kudhibiti na kuzima moto uliokuwa umeteketeza magari hayo.
Katika hatua nyingine, Michel Benjamin ambaye pia ni dereva na shuhuda wa tukio hilo, ameeleza kuwa safari yao ilikuwa ikiendelea kawaida kabla ya kushuhudia ajali hiyo ya kutisha, akieleza kuwa tukio hilo liliibua hofu na taharuki kubwa miongoni mwa watumiaji wengine wa barabara hiyo.
Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.