Mwanza. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza imefanikiwa kudhibiti Sh85 milioni zilizokuwa zimecheleweshwa kutolewa kwa walimu wapya 77 wa shule za sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa miezi sita.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Februari 25, 2026 Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Abnery Mganga amesema katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, jumla ya walimu 77 waliokuwa wamepangiwa kazi katika Jiji la Mwanza walicheleweshewa malipo yao ya kujikimu, jambo lililosababisha malalamiko na hofu miongoni mwao, baadhi wakidhani huenda fedha hizo zilikuwa zimepotea au kuibiwa.
Amesema mafanikio ya kudhibiti fedha hizo yametokana na kazi ya uchambuzi wa mfumo wa malipo ya fedha za kujikimu kwa walimu wapya walioajiriwa na Serikali na kupangwa katika halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Mwanza.
“Kama mtakumbuka hivi karibuni Serikali iliajiri walimu wapya wa shule za sekondari. Kwa hiyo jumla ya walimu 77 walicheleweshewa malipo yao ya kujikimu…kwahiyo yaliibuka malalamiko mengi na kuonekana fedha hizo kama zimeibiwa, sasa Takukuru ilingilia kati na kuwezesha fedha hizo zote kupatikana na kisha kulipwa kwa walimu hawa,”ameeleza.
Nakuongeza, “Kumbuka walimu hawa walicheleweshewa fedha hizi kwa zaidi ya miezi sita kwahiyo kidogo ilikuwa inaleta sintofahamu lakini kwa intervation ya Takukuru (kuingilia kati) kazi hii ilifanyika na walimu wote wakalipwa fedha zao,”
Amesema mafanikio hayo ni baada ya taasisi hiyo kufanya uchambuzi wa mfumo na Halmashauri kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa kwenye kikao cha warsha baina ya Takukuru na wadau wa Halmashauri na hivyo kusaidia walimu hao 77 waliokuwa na madai kulipwa stahiki zao.
Akizungumzia hatua zilizochukiliwa Mganga amesema“Kimsingi fedha ilicheleweshwa kwenye akaunti ya Mkurugenzi baada ya kuwa Serikali ilitoa ilitakiwa fedha ile ilipwe moja kwa moja. Sasa kwakuwa hakukuwa na vitendo vya rushwa..haikuwa rushwa moja kwa moja ya kuchukua hatua za kisheria,
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Abnery Mganga akizungumza na waandishi wa habari. Picha na Saada Amir
“Haikukuwa na ushahidi wa kwamba fedha hiyo iliibwa au kuhamishwa ikafanye majukumu mengine ni fedha tu ilifika kwenye akaunti ikacheleweshwa..hatua tulizochukua sisi ni hizo za kufanya uchambuzi wa mifumo na kudhibiti fedha hizo pengine ucheleweshwaji ule ungeweza kuleta kero zaidi ama kuleta changamoto nyingine ambayo ingesababisha vitendo vya rushwa,”
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba kuzungumzia ucheleweshwaji huo amejibu hana taarifa ya walimu hao kucheleweshewa malipo yao ya kujikimu na kwamba ndiyo kwanza kaisikia kwa mwandishi wa habari.
Mbali na kudhibiti fedha hizo, jumla ya miradi 17 yenye thamani ya Sh4.7 bilioni ilifuatiliwa kwa lengo la kuhakikisha inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha ambapo mapungufu madogomadogo yaliyobainika, kutolewa mapendekezo ya kuboresha na wahusika walitekeleza maelekezo hayo.
Mkuu huyo wa Takukuru amesema katika eneo la elimu kwa umma zaidi ya wananchi 7,000 wakiwemo watumishi wa umma, sekta binafsi, vijana, wanawake na wazee walipatiwa elimu kuhusu madhara ya rushwa na umuhimu wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
“Elimu hiyo imeongeza uelewa na kuimarisha ushirikiano kati ya Takukuru na wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa,”amesema.
Amesema taarifa 59 zilipokelewa katika robo hiyo, ambapo 24 zilihusu tuhuma za rushwa na 35 hazikuhusu rushwa.
“Taarifa zinazohusu Rushwa uchunguzi umeanzishwa, zisizohusu rushwa ushauri umetolewa na nyingine kuwasilishwa kwenye Taasisi za mamlaka husika kwa ajili yakufanyiwa kazi,” ameeleza.