Global Publishers
February 26, 2026
0 Comments
Usiku wa kuamkia leo Februari 26, 2026 michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya umeshuhudia vigogo kadhaa wakifuzu hatua ya 16 bora baada ya michezo ya mchujo (playoffs), huku pambano la Juventus dhidi ya Galatasaray likiendelea kuandika historia kwa kuelekea dakika 30 za nyongeza kufuatia sare ya jumla.
Real Madrid waliendeleza rekodi yao ya kuwa mabingwa wa usiku wa Ulaya baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Benfica, ushindi uliowapa tiketi ya kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-1.
Benfica walipata bao la mapema kupitia Rafa Silva dakika ya 14, lakini wenyeji hawakuyumba. Aurelien Tchouameni alisawazisha dakika ya 16 kabla ya Vinicius Jr kupachika bao la ushindi dakika ya 80. Madrid walionekana kuwa na udhibiti mkubwa wa mchezo, wakithibitisha uzoefu wao katika hatua za mtoano.
Katika pambano la wababe wa Ufaransa, PSG walilazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Monaco, lakini wakafuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-4.

Monaco walitangulia kupitia Akliouche dakika ya 44, kabla ya PSG kugeuza upepo kipindi cha pili kupitia Marquinhos na Kvaratskhelia ndani ya dakika sita. Bao la kusawazisha la Teze dakika za majeruhi liliongeza presha, lakini halikutosha kuiondoa PSG katika mashindano.
Atalanta waliandika ukurasa mpya wa mafanikio baada ya kuichapa Dortmund mabao 4-1 na kufuzu kwa jumla ya mabao 4-3.
Scamacca alifungua ukurasa mapema dakika ya tano, Zappacosta akaongeza la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Kipindi cha pili kilishuhudia Pasalic na Samardzic (kwa mkwaju wa penalti) wakihitimisha kazi hiyo. Bao la Adeyemi kwa Dortmund halikubadili hatima ya mchezo.