Fountain, Namungo Ligi Kuu ya NBC, mechi ya mipango

WAKATI leo Alhamisi Fountain Gate na Namungo zikiwa viwanja tofauti kusaka pointi Ligi Kuu Bara, unaweza kusema  hali ni tete kwa timu hizo ndani ya raundi tano zilizopita sawa na dakika 450 zimeshindwa kuibuka na ushindi.

Katika mechi tano zilizopita, Yanga ndiyo iliyokusanya pointi nyingi zaidi ambazo ni 15 (kabla ya mechi ya jana) dhidi ya Namungo (1-0), Dodoma Jiji (3-1), Mashujaa (6-0), Coastal (1-0) na Fountain Gate (2-0).

Fountain Gate na Namungo zimeambulia pointi mbili kati ya 15 kila moja kuchapwa mechi tatu na sare mbili.

Kipigo ambacho Namungo ilikumbana nacho dhidi ya Yanga Jumapili iliyopita kilikuwa cha tatu mfululizo baada ya kile cha Tanzania Prisons 3-2 na Pamba Jiji 1-0.

Kabla ya hapo kilitoka sare mbili dhidi ya Mtibwa na Fountain Gate kwa bao 1-1 katika kila mechi.

Kwa upande wa Fountain Gate ambayo ipo nafasi ya 15 kati ya timu 16 mara ya mwisho ilifungwa bao 1-0 na Singida Black Stars lakini kabla ya hapo sare mbili mfululizo dhidi ya Namungo 1-1 na Azam 0-0.

Katika mechi mbili za kwanza ilipoteza dhidi ya Yanga na JKT Tanzania katika kila mechi 2-0.

Pamoja na Fountain Gate na Namungo kuwa zilizofanya vibaya katika mechi tano zilizopita, KMC inayoburuza mkia ikiwa na pointi nane katika mechi 16 ndiyo timu iliyopoteza mechi nyingi zaidi katika raundi tano zilizopita imechapwa nne na kushinda moja.

Vijana hao wa Kinondoni, wamepoteza mbele ya Azam FC na Simba kila mechi kwa mabao 2-0, Dodoma Jiji kwa mabao 2-1 na Namungo kwa bao 1-0, imeshinda dhidi ya Mashujaa kwa bao 1-0. Kwenye Uwanja wa Black Rhino uliopo Karatu mkoani Arusha, Fountain Gate leo itaikaribisha TRA United katika msako wa pointi tatu, mechi ikipangwa kuanza saa 10:00 jioni.

Baada ya mechi hiyo, saa 1:00 usiku Namungo itaikaribisha Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa mkoani Lindi.