Ulega: Babarara Mlima Kitonga kuwa njia nne 

Serikali iko katika hatua za mwisho za kuanza upanuzi wa barabara ya Kitonga mkoani Iringa, ambayo sasa itakuwa ya njia nne na yenye taa za barabarani. Mkakati huo unatajwa kuwa licha ya kuboresha huduma, lakini pia unakwenda kumaliza ajali kwenye eneo hilo.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametangaza mpango Jumatano, Februari 26, 2026 na kuwa hatua hiyo ni uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kupunguza foleni na kuboresha usalama wa watumiaji barabara katika njia hiyo inayotumiwa na magari mengi.

Waziri Ulega aliyekuwa katika ziara ya ukaguzi wa eneo la zaidi ya kilomita saba linalopaswa kupanuliwa, amesema barabara hiyo ni ya kimkakati kwa uchumi wa nchi kwa sababu inatumiwa pia na magari yanayokwenda katika nchi zinazotumia Bandari ya Dar wa Salaam kubeba mizigo yao.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akizungumza wakati alipofanya ziara eneo la Mlima Kitonga mkoani Iringa ambako, Serikali imetengaza kujenga njia nne ili kupunguza msongamano na kudhibiti ajali. Na Mpigapicha Wetu



“Barabara hii sasa itakuwa ya njia nne- mbili za kwenda na mbili za kurudi ambapo sasa ni njia mbili tu zinatumika. Na tutafunga taa kote ili kuhakikisha muda wote barabara inapitika muda wote,“ amesema Ulega.

Akitoa picha ya ongezeko la uhitaji wa upanuzi  wa barabara hiyo, mbunge huyo wa Jimbo la Mkuranga alisema idadi ya magari yanayopita katika Barabara Kuu ya TANZAM imeongezeka kutoka magari 1,700 hadi 3,400 kwa siku, hali inayopelekea barabara hiyo kuzidiwa na wingi wa magari.

“Nimepokea mapendekezo kutoka kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa ya kuhakikisha tunaondoa msongamano wa magari katika mlima Kitonga, na nimeelekeza kwa wataalamu wetu kupanua hii barabara kwa kilometa saba. Kwa sasa hivi barabara ina njia mbili kwa hiyo tutatanua na kuwa njia nne,” amesema Ulega.

Waziri Ulega ameongeza kuwa ni maelekezo ya Rais Samia kwamba kila mradi wa barabara uende sambamba na uwekaji wa taa za barabarani ili kuhakikisha usalama wa watumiaji ikiwemo wananchi, wafanyabiashara na madereva pamoja na kuweka kingo pembezoni mwa barabara ili kuzuia magari yasianguke kwenye makorongo.


“Ninaagiza manunuzi yaanze mara moja ili kuhakikisha kwamba barabara hii inatanuliwa kwani, ina umuhimu mkubwa katika uchumi wa nchi hivyo hatuwezi kuiacha katika hali hii na kutimiza pia maelekezo ya Mheshimiwa Rais kutatua changamoto zote,” ameongeza Waziri Ulega.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Ritha Kabati, amesema barabara hiyo ni ya uchumi wa kimataifa hivyo ikitengenezwa itainua zaidi uchumi wa mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla pamoja na kuwasaidia wananchi ambao, hupata changamoto ya kufuata huduma za kijamii ikiwemo matibabu Iringa mjini.


Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa, Mhandisi Yudas Msangi amesema gharama ya upanuzi wa kilometa saba wa njia mbili katika barabara hiyo ni Sh59.2 bilioni na ukarabati wa njia mbili zilizopo ni Sh16.2 bilioni.