GEPU la pointi tano baina ya vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga dhidi ya Simba inayoshika nafasi ya tatu, ni miongoni mwa vitu vinavyokwenda kunogesha Dabi ya Kariakoo.
Zikiwa zimebaki takribani siku tatu kabla ya kucheza mechi hiyo Machi Mosi 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Yanga imeendelea kuthibitisha ubora katika Ligi Kuu Bara baada ya kuibuka na ushindi wa nane mfululizo ikiichapa JKT Tanzania mabao 5-0, jana Jumatano kwenye Uwanja wa KMC, Dar.
Ushindi huo unaifanya Yanga kwenda kwenye Dabi ya Kariakoo ikiwa kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi 28.
Kwa upande wa Simba yenye pointi 23, jana Jumatano ilishindwa kufungana na Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma. Kabla ya mechi hizo za jana, tofauti ya pointi baina ya Yanga na Simba zilikuwa tatu huku zote sasa zikicheza mechi sawa ambazo ni kumi.
Presha kubwa ipo kwa Simba kwani ikitokea imepoteza au kutoka sare dhidi ya Yanga, kuna hatari ikashushwa na Azam yenye pointi 22 kwa sasa endapo itashinda mechi yake ijayo Machi 2, 2026 dhidi ya Pamba Jiji ikiwa ugenini.
Jana Yanga ilituma salamu za Dabi ya Kariakoo ilipoichapa JKT Tanzania mabao 5-0, huku mechi hiyo ikionekana kuwa ngumu mwanzoni, lakini baadaye, ikawa laini kwa mabingwa hao watetezi.
Dakika ya saba tu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alifunga bao akimalizia pasi ya Prince Dube. Bao hilo liliwapa utulivu na kujiamini Yanga ambao walimiliki mpira na kutengeneza nafasi zaidi za kufunga.
Yanga ilinda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuongeza kasi na kufanya mabadiliko madogo kwa kuingia Mohamed Damaro na kutolewa Allan Okello, mabadiliko hayo yaliimarisha eneo la kiungo. Mudathir Yahya alianza kuonekana zaidi katika mashambulizi, akiunganisha safu ya kati na ushambuliaji.
Dakika ya 61, Depu alipachika bao la pili kwa kichwa, likiwa ni bao lake la tano msimu huu katika ligi hiyo. Dakika mbili baadaye, Mudathir Yahya aliongeza la tatu na kuzidi kuwakatisha tamaa maafande hao.
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alitumia nafasi hiyo kuwapumzisha baadhi ya nyota wake, lakini kasi ya timu haikupungua. Dakika ya 85, Prince Dube alifunga bao la nne kabla ya Shekhani Khamis kuhitimisha ushindi huo kwa bao la tano.
Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 28, sawa na JKT Tanzania lakini imekaa kileleni kwa tofauti ya mabao.
Tangu ilipotoka sare ya 0-0 dhidi ya Mbeya City Septemba 30, 2025, Yanga imeshinda mechi nane mfululizo za Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar (2-0), KMC (4-1), Fountain Gate (2-0), Coastal Union (1-0), Mashujaa (6-0), Dodoma Jiji (3-1), Namungo (1-0) na JKT Tanzania (5-0).
Jumapili Machi Mosi 2026, Yanga itaikaribisha Simba katika Dabi ya Kariakoo ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.
Benchi la Ufundi la Simba likiongozwa na Kocha Mkuu, Steve Barker, lilikuwa likifahamu kwamba kikosi chao kinaingia uwanjani kikiwa na deni la kupunguza gepu la pointi dhidi ya Yanga, lakini Dodoma Jiji ikaitibulia kwa mara ya kwanza tangu kuanza kukutana kwao.
Mechi hiyo iliyokuwa ya ushindani mwanzo hadi mwisho na kumalizika kwa suluhu (0-0), muda mwingi wachezaji waliopambana kwa kasi, nguvu na ubabe wa hapa na pale ambapo Simba licha ya kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini uimara wa kujilinda wa kikosi cha Dodoma Jiji uliinyima kuondoka na pointi tatu.
Simba iliingia ikiwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya Dodoma Jiji, kwani mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu, ilishinda mabao 6-0, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Machi 14, 2025.
Sare ya jana ilikuwa ya kwanza kwa Dodoma Jiji dhidi ya Simba, kwani kikosi hicho tangu kianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2020-2021, kilikuwa hakijashinda wala kutoka sare, zaidi ya kuambulia vichapo kumi mfululizo.
Matokeo hayo, yameifanya Dodoma Jiji kuendelea kubaki nafasi ya sita kwa pointi 21, baada ya kucheza mechi 16, kati ya hizo imeshinda tano, sare sita na kupoteza tano, ikifunga mabao 14 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15.
Kwa upande wa Simba ipo nafasi ya tatu kwa pointi 23, baada ya kushinda mechi saba, sare mbili na kupoteza moja kati ya 10 ilizocheza, huku ikifunga mabao 18 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne.
Baada ya watani hao wa jadi kucheza mechi mbili za ligi tangu kutoka mashindano ya kimataifa, kituo kinachofuta ni Dabi ya Kariakoo ambayo matokeo ya ushindi kwa Yanga yatamaanisha inaiacha Simba parefu, lakini ikiwa kinyume chake, pengine inaweza kuwa mwanzo mzuri wa Simba kufuta uteja.
Rekodi zinaonyesha, Yanga imeifunga Simba mara sita mfululizo katika kukutana kwao hivi karibuni kwenye mashindano tofauti ambapo Ligi Kuu mechi nne na Ngao ya Jamii mbili.
Mara ya mwisho Simba kuifunga Yanga ilikuwa katika Ngao ya Jamii iliyochezwa Agosti 13, 2023 kwa penalti 3-1.
Baada ya hapo, matokeo ya Ligi Kuu Bara yalikuwa hivi; Simba 1-5 Yanga (Novemba 5, 2023), Yanga 2-1 Simba (Aprili 20, 2024), Simba 0-1 Yanga (Oktoba 19, 2024) na Yanga 2-0 Simba (Juni 25, 2025). Pia mechi mbili za Ngao ya Jamii matokeo yalikuwa hivi; Yanga 1-0 Simba na Yanga 1-0 Simba.