UMBALI MREFU SABABU YA WANAFUNZI KUTOFANYA MTIHANI

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Biharamulo, Innocent Mkandara.

……….

IMEELEZWA kuwa umbali mrefu wa kufika shuleni pamoja na wazazi kuhama makazi yao ya awali pasipo kutoa taarifa rasmi za wanafunzi wanaosoma shule za msingi wilayani Biharamulo mkoani Kagera ni chanzo cha kuporomoka kwa idadi ya watahiniwa wa darasa la nne.

Hayo yamesemwa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Innocent Mkandara, wakati akijibu hoja ya Diwani wa kata ya Nyanza, Leo Rushahu, aliyetaka kujua sababu za watoto takribani 1,157 kushindwa kufanya mtihani wa upimaji wa darasa la nne kwa mwaka 2024.

Hoja hiyo imeibuliwa kwenye kikao cha Baraza la madiwani katika mjadala wa mpango na bajeti ya mwaka 2026/27 huku Baraza hilo likijikita kupitia kwanza mafanikio na changamoto za bajeti ya mwaka 2024/25 na 2025/26.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, ilionyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2024, jumla ya wanafunzi 12,604 kati ya 13,761 ndiyo waliofanya mtihani wa upimaji wa darasa la nne ambayo ni sawa na aslimia 87.8 pekee.

Kutokana na hali hiyo, wajumbe wa Baraza hilo wakataka kujua sababu zilizosababisba baadhi ya wanafunzi kutofanya mtihani huo.

Mbali na hilo, ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali, halmashauri hiyo imeendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato kwenye vituo mbalimbali vya umma kwa kutumia mfumo wa “Gothomis” iliyobireshwa.

Hata hivyo, suala la upatikanaji wa watoa huduma kupitia mfumo wa manunuzi ya umma (Nest) umeendelea kuumiza vichwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Ni kutokana na Wazabuni na mafundi wanaoomba kazi kwenye mfumo huo kuwa ni wachache sana ukilinganisha na zabuni zinazotangazwa.

                         Mwisho.