Video: Magari Yagongana Uso kwa Uso Na Kuwaka Moto, Mmoja Afariki

Bakari Mahundu
February 26, 2026
0 Comments

Mtu mmoja amefariki dunia na watu wawili kujeruhiwa baada ya magari mawili ya kubeba mizigo kugongana uso kwa uso na kuteketea kwa moto katika kijiji cha Kiongozi, kata ya Maisaka, wilayani Babati mkoani Manyara. Ajali hiyo imetokea leo Februari 26, 2026.

Akizungumza akiwa eneo la tukio, Inspekta wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo, Gilbert Mushi, amesema walipokea taarifa za ajali hiyo na kufika eneo la tukio kwa ajili ya shughuli za uokoaji na udhibiti wa moto.

Mushi ameeleza kuwa magari yaliyohusika katika ajali hiyo yalikuwa yakitokea pande tofauti, moja likifanya safari kutoka Rwanda kuelekea Tanga, huku jingine likitokea Arusha kuelekea kanda ya kaskazini likiwa na mzigo wa bia. Alifafanua kuwa magari hayo yalipokutana katika eneo lenye mtelemko, yaligongana uso kwa uso na kusababisha moto kuwaka.

Kwa upande wao, mashuhuda wa ajali hiyo wamesema ajali ilitokea ghafla, huku wakieleza juhudi walizozifanya kuwatoa majeruhi katika magari hayo licha ya moto kuwa ukiendelea kuwaka.