Songwe. Kaya zenye vyoo bora wilayani Ileje Mkoani Songwe zimefikia asilimia 54 sawa na kaya 9,950 huku asilimia 0.2 sawa na kaya 234, hazina vyoo kabisa huku wananchi wakihimizwa kutumia vyoo vya kisasa kwa usalama wa afya zao.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Februari 26, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi wakati wa hamasa ya kampeni ya kuhamasisha wananchi kujenga vyoo vya kisasa, hafla iliyofanyika katika Kata ya Bupigu wilayani humo.
Mgomi amesema hamasa hiyo ni sehemu ya mradi unaodhaminiwa na EEPCO kwa kushirikiana na UNICEF, ukiwa na lengo la kuboresha hali ya usafi na mazingira katika ngazi ya kaya.
Amesema mradi huo umeendelea kuleta mwamko chanya kwa wananchi katika kubadili mitazamo na kuchukua hatua madhubuti za kulinda afya zao.
Mgomi amesisitiza kuwa suala la afya si hiari bali ni wajibu wa kila mwananchi, akiwataka kuzingatia matumizi sahihi ya vyoo pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
Mkuu wa wilaya ya Ileje, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa vijiji na kata katika hamasa ya ujenzi wa vyoo bora. Picha na Denis Sinkonde
“Mpaka sasa Wilaya ya Ileje ina kaya 9,950 sawa na asilimia 54, hutumia vyoo vya kisasa, kaya 8,270 sawa na asilimia 44 wanatumia vyoo vya kienyeji, kaya 234 sawa na asilimia 0.4 hawana vyoo kabisa,” amesema Mgomi.
Amesema kaya 8,203 sawa na asilimia 44.5 hutumia maji tiririka na kaya 7,328 wanatumia vifaa vya kunawia na sabuni.
“Ni jukumu la kila sekta kuhakikisha ufuatiliaji wa kina unafanyika katika ngazi zote kuanzia kaya , shule, vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na taasisi ili kutilia mkazo ujenzi na matumizi bora ya vyoo,” amesema Mgomi.
Aidha, amezitaka mamlaka za vijiji na kata na ngazi ya wilaya kushirikiana kwa karibu na wananchi ili kuhakikisha usafi wa mazingira, ikiwemo ujenzi na matumizi ya vyoo bora unazingatiwa kikamilifu.
Amesema ni muhimu kila kaya kuhakikisha inajenga na kutumia choo bora kuondokana na magonjwa yanayotokana na uchafu yakiwemo magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
Amesisitiza kuwa ushirikiano huo utasaidia kujenga jamii yenye afya bora na mazingira salama kwa maendeleo endelevu ya Wilaya ya Ileje.