Mahakama yasimamisha usikilizwaji kesi ya uteuzi wabunge viti maalumu

Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Dodoma, imesitisha kwa muda usikilizwaji wa shauri la mapitio ya kimahakama lililofunguliwa na ACT-Wazalendo kupinga uteuzi wa wabunge wa viti maalumu uliofanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Uamuzi huo umetolewa jana Februari 25, 2026 na Jaji Griffin Mwakapeje baada ya wajibu maombi kueleza kuwa kuna shauri la mapitio (revision) lililofunguliwa katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania kupinga ruhusa iliyotolewa kufungua shauri hilo la msingi.

Serikali, kupitia Wakili Mkuu, Vivian Method, ilidai kuwa iwapo ruhusa hiyo itabatilishwa, basi shauri la msingi litakosa uhalali wa kisheria. Upande wa ACT, kupitia Wakili John Seka, ulipinga kusitishwa kwa shauri hilo ukisema hakuna kifungu kinachoelekeza kusimamishwa moja kwa moja.

Katika uamuzi wake, Jaji alisema Mahakama haiwezi kuendelea wakati suala la mamlaka yake liko chini ya uchunguzi wa mahakama ya juu. Hivyo, shauri namba 705/2026 litasubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufani kabla ya kuendelea.