Dar es Salaam. Mkazi wa Kibamba, Hakeem Palangyo, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kugushi barua za vyuo vikuu.
Palangyo amefikishwa mahakamani hapo leo, Alhamisi, Februari 26, 2026, na kusomewa kesi yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube.
Akimsomea shtaka, wakili wa Serikali, Bony Lawrence, amedai kuwa Februari 13, 2018, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa huyo aligushi barua ya tarehe hiyo na Septemba 13, 2028, akionesha kuwa ni halali zimetolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), wakati akijua si kweli.
Lawrence aliendelea kudai kuwa Oktoba 11, 2018, Palangyo alitoa barua ya Februari 13, 2028, katika Chuo cha Iringa, akidai ni halali imetolewa na TCU.
Pia ilidaiwa kuwa Februari 11, 2019, mshtakiwa huyo alitoa barua ya Septemba 13, 2018, katika Chuo cha Mtakatifu Joseph, akidai ni halali imetolewa na TCU, wakati si kweli.
Mshtakiwa amekana tuhuma hizo, upande wa mashtaka umedai upelelezi umekamilisha. Kesi imeahirishwa hadi Machi 11, 2026, kwa ajili ya kusomwa hoja za awali.
Mshtakiwa amepelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ambayo ni kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.