Njombe. Wananchi wa vijiji saba wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe, wamepatiwa miche 700 ya miti kwa lengo la kuwasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hali inayotajwa kuathiri uzalishaji wa mazao na kupunguza tija kwa wakulima wa eneo hilo.
Mabadiliko ya tabianchi yameelezwa kuwa chanzo cha ardhi kupoteza rutuba, jambo linalowalazimu wakulima kutumia kiasi kikubwa cha mbolea ili kuongeza uzalishaji na kupata faida.
Akizungumza leo Alhamisi Februari 26, 2026, wakati wa hafla ya kukabidhi miche hiyo iliyofanyika Wanging’ombe, Mkuu wa Idara ya Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Kasmiri David amesema mabadiliko hayo yameathiri pia kiwango na mpangilio wa mvua, hali inayochangia kupungua kwa virutubisho kwenye ardhi.
Amesema upotevu huo wa rutuba unasababisha wakulima kutumia mbolea nyingi zaidi katika uzalishaji wa mazao yao ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
“Zamani hali ya hewa ilipokuwa nzuri, wakulima walitumia mbolea kwa kiwango kidogo na bado walipata mavuno mazuri. Lakini sasa mabadiliko ya tabianchi yamesababisha upotevu wa virutubisho kwenye ardhi na hata kwenye mazao tunayozalisha,” amesema David.
Ametaja uharibifu wa mazingira, hususan kupotea kwa uoto wa asili na ukataji holela wa miti, kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kuongezeka kwa joto na kuharakisha athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, amewataka wananchi kuacha tabia ya kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa, akisisitiza umuhimu wa kuitunza miche waliyopewa ili iweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo Mkoa wa Njombe (NADO), Jonathan Ngilangwa, alisema ugawaji wa miche hiyo ni sehemu ya jitihada za kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Siyo jambo jipya kwetu kugawa miche ya miti. Mwaka juzi na mwaka jana tulifanya hivyo, hata katika shule za msingi. Lengo ni kuhamasisha jamii ichukue hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Ngilangwa.
Naye Mratibu wa Mradi wa Uhifadhi wa Mazingira kutoka NADO, Ernest Ng’umbi, alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026 shirika hilo limezalisha miche 99,300, ikiwemo inayosaidia kurejesha rutuba shambani.
Amefafanua kuwa uzalishaji wa miche hiyo huzingatia ukanda wa kijiografia wa mkoa wa Njombe, ambao umegawanyika katika kanda ya juu, ya kati na ya chini, ili kuhakikisha miti inayozalishwa inaendana na mazingira ya kila eneo.
Baadhi ya wananchi walionufaika na mpango huo, akiwemo Jacob Nyagawa, walisema mabadiliko ya tabianchi yameongeza gharama za uzalishaji wa mazao kutokana na hitaji la kutumia mbolea na viuatilifu kwa wingi katika kila hatua ya ukuaji wa mimea.
“Kuna changamoto ya kutumia dawa nyingi kuokoa mimea ili iweze kukua, kwa sababu virutubisho kwenye ardhi vimepungua,” amesema Nyagawa.