Zaidi ya watu 60,000 kunufaika na mpango wa bima ya afya Shinyanga

Shinyanga. Watu 63,541 mkoani Shinyanga wanatarajia kunufaika na mpango wa Bima ya Afya kwa wote ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha huduma za afya na kuhakikisha kila mwananchi anapata matibabu ya uhakika.

Hayo yameelezwa leo Februari 26, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC),

Mhita amesema utekelezaji wa mpango huo unaenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha.

Wajumbe wakiwa kwenye kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita.



“Lengo letu ni kuona kila mwananchi anakuwa na uhakika wa kupata matibabu anapougua, hii ni hatua muhimu katika kuboresha ustawi wa jamii na kuondoa vikwazo vyote kwa wananchi kwenye huduma,” amesema Mhita.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa amesema suala la utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu linaendelea kutekelezwa kwa mujibu wa miongozo ya Serikali.

Ameeleza kuwa mikopo hiyo inalenga kuyawezesha makundi hayo kiuchumi ili kuongeza kipato chao na kuchangia maendeleo ya mkoa, ikiwa ni pamoja na kuwaepusha wananchi na mikopo kausha damu ambayo inawaumiza wananchi.

Wajumbe wakiwa kwenye kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita.



Aidha, amepongeza juhudi zinazoendelea katika kuboresha huduma za maji mijini na vijijini, akieleza kuwa upatikanaji wa maji safi na salama umeimarika kwa kiwango kikubwa ambapo Serikali itaendelea kusimamia miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma hiyo.

Mdau wa maendeleo mkoani Shinyanga, Salima John amesema bima ya afya kwa wote itawawezesha wananchi ambao wanatoka kaya ambazo hazina uwezo kupata matibabu kupitia kadi za bima zilizolipiwa na Serikali.