Arusha. Wakati ripoti ya kimataifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ikionyesha wanaume duniani wanaongoza kwa vifo vya mapema, takribani asilimia 13 zaidi ya wanawake kila mwaka, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imezindua mkakati mahsusi wa kuhamasisha uchunguzi wa mapema wa afya ya moyo ili kupunguza vifo vya mapema, hususan miongoni mwa wanaume.
Kwa mujibu wa WHO, wanawake huishi kwa wastani wa miaka 73.8 ikilinganishwa na miaka 68.4 kwa wanaume na hivyo kuacha pengo la takribani miaka mitano hadi saba kati ya jinsia hizo.
Tofauti hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na hatari wanazokumbana nazo wanaume katika maisha yao, ikiwemo magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, pamoja na mtindo wa maisha usiozingatia kanuni bora za afya.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 26, 2026, katika kambi ya matibabu ya mifupa na ubongo, Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali ya JKC-ALMC (Arusha Lutheran Medical Centre) inayosimamiwa na JKCI, Dk Saleh Hamis Mwinchete, amesema suluhisho la msingi ni wanaume kuweka utaratibu wa kufanya uchunguzi na vipimo vya afya mara kwa mara, hata wanapokuwa hawana dalili zozote.
“Hii inasababishwa kwa kiasi kikubwa na wanaume kutokuwa na desturi ya kuhudhuria hospitalini kwa uchunguzi wa mara kwa mara, ambapo wengi hufika wakiwa tayari katika hatua za juu za ugonjwa, hasa magonjwa ya moyo, jambo linalofanya matibabu kuwa ya gharama kubwa au kuhitaji huduma za kibingwa zaidi,” amesema.
Dk Mwinchete amesema kuwa kutokana na zaidi ya asilimia 80 ya vifo duniani vinatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, huku magonjwa ya moyo yakichangia takribani asilimia 74 ya vifo hivyo, ndiyo maana wameamua kuja na kampeni hiyo ya kuhamasisha upimaji wa mapema ijulikanayo ‘zijue namba zako’.
Amesema magonjwa ya moyo mara nyingi hayana dalili katika hatua za awali, hali inayofanya wengi kugundulika wakiwa tayari katika hatua hatarishi.
“Hii ndio mbaya zaidi ndiyo maana tunasisitiza uchunguzi wa mapema maana ukigundua mapema, unapata matibabu kwa gharama nafuu, unakuwa na uhakika mkubwa wa kupona na kuendelea na maisha ya kawaida,” amesema.
Amesema katika utekelezaji wa kampeni hiyo, wameandaa kambi ya siku saba za upimaji na matibabu bure ya magonjwa ya moyo itakayoanza kesho Februari 28 hadi Machi 6, 2026 katika hospitali ya JKC-ALMC iliyoko Arusha mjini.
Amesema huduma za uchunguzi wa awali zitatolewa bure huku watakaobainika kuwa na changamoto wakipatiwa matibabu kwa gharama nafuu na jopo la madaktari kutoka nchini na nchi ya Misri.
“Katika kambi hii ya JKC-ALMC inatarajia kuhudumia zaidi ya watu 1,000 katika kipindi cha siku hizo saba, kwa kushirikiana na wataalamu zaidi ya saba wa magonjwa ya moyo kutoka JKCI, JKC-ALMC pamoja na kutoka Misri,” amesema.
Akizungumzia kambi ya matibabu ya mifupa na ubongo kwa watu wazima na watoto, Kaimu Mkurugenzi wa tiba na mifupa kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dk Emmanuel Lema amesema wameanza huduma hiyo Jumatatu Februari 23, 2026 na itatamatika kesho Februari 27, 2206
Amesema zaidi ya watu 720 wamehudumiwa huku upasuaji wa wagonjwa 20 ukiwa tayari umefanyika kwa ushirikiano kati ya JKCI na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).
“Hadi kufikia mwisho wa kambi hiyo, jumla ya wagonjwa 1,200 wanatarajiwa kuhudumiwa na zaidi ya upasuaji 30 kufanyika kulingana na miadi iliyopangwa hadi sasa,” amesema.
Mmoja wa wanufaika, Neema Kiriko amesema alisumbuliwa kwa muda mrefu na maumivu makali ya magoti na kulazimika kutumia dawa za maumivu bila mafanikio, lakini kupitia kambi hiyo amefanyiwa upasuaji na sasa ana matumaini ya kurejea katika hali yake ya kawaida.
Ametoa rai kwa taasisi za afya kuendelea kuandaa kambi za matibabu mara kwa mara ili kupunguza gharama kwa wananchi wanaolazimika kusafiri hadi Dar es Salaam kufuata huduma za kibingwa.