Dar es Salaam/Kiteto. Ziara ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, wilayani Kiteto mkoani Manyara imekuwa kaa la moto kwa kwa watumishi wa umma na wasimamizi wa miradi ya maendeleo mkoani humo, baada ya kubaini kile alichokiita, ‘mchezo mchafu’ wa kugawana fedha za umma zilizotengwa kwa miradi.
Akizungumza mbele ya viongozi na wananchi, Dk Nchemba ambaye ameanza ziara leo Februari 26, 2026, amesema ana taarifa kuwa Kiteto ni miongoni mwa maeneo ambayo ‘mchezo mchafu’ umefanyika.
Akiwa katika shughuli ya uwekaji jiwe la msingi la jengo la ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Waziri Mkuu amesema alikuwa akifuatilia kwa karibu mwenendo wa miradi kabla ya kufika Kiteto na kubaini dalili za baadhi ya viongozi kujaribu kumwelekeza kwenye miradi iliyopangwa pekee.
“Nilikuwa nawaangalia tu mnavyohangaika mnipeleke kwenye mradi gani. Nani kawaambia mimi nimekuja kutembea hapa? Nina taarifa zote za kilichofanyika kwenye jengo hili na nina taarifa zote kuhusu kilichofanyika kwenye jengo la halmashauri ambalo hamjanipeleka.
“Hapa zililetwa fedha za mradi, watu wamegawana katika kukimbizana, ndiyo wakarudisha fedha hii iliyotumika kukamilisha ujenzi wa jengo la mkuu wa wilaya, kwa hiyo walishatuibia tusingewaona,” amesema.
Kutokana na tuhuma hizo, Dk Nchemba amemwagiza Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Manyara, Bahati Haule kufanya uchunguzi na kuwasilisha taarifa ya kina ya kila mhusika na kiwango cha ushiriki wake kabla hajamaliza ziara yake mkoani humo.
“Niletee taarifa za mmoja mmoja na ushiriki wake, lazima hatua za kisheria zichukuliwe. Hatuwezi kuwa na mambo ya kipuuzi namna hii. Niipate taarifa hii kabla sijamaliza ziara Mkoa wa Manyara,” amesema.
Sambamba na uchunguzi huo, amemuagiza waziri mwenye dhamana kupeleka suala hilo Tume ya Maadili ya Watumishi wa Umma ili kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wa umma waliobainika kuhusika, hata kama walisharejesha fedha hizo.
“Wale waliochukua fedha pamoja na kurudisha, waziri wapeleke tume ya maadili ili hatua za kinidhamu zichukuliwe. Haya mambo ya watu kupata nafasi halafu wakajiona bora zaidi ya Watanzania wengine hayakubariki. Fedha za miradi zitumike kama zilivyopangwa,” amesema.
Amesisitiza kuwa, fedha za maendeleo si siri na hazipaswi kufichwa kwa kigezo chochote, akionya kuwa kufanya hivyo ni kutengeneza kichaka cha ufisadi.
“Kuanzia sasa fedha za miradi zikifika kwenye mkoa, nakala apewe mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya hadi madiwani. Fedha za maendeleo si siri. Kinyume na hivyo ni watu kutengeneza vichaka vya kuiba na kujinufaisha. Hili halikubaliki,” amesema.
Waziri Mkuu ameonya kuwa, hatavumilia uzembe, uvivu na wizi wa mali ya umma, akisisitiza kuwa, hakuna kufanyiana ustaarabu linapokuja suala la rasilimali za wananchi.
“Nachukia uzembe, uvivu na wizi, hata kama tuko kwenye Kwaresma na mwezi mtukufu, hawa lazima watapata cha moto. Hakuna kufanyiana ustaarabu kwenye mali ya umma,” amesema.
Waziri Mkuu kuwa ametaka taarifa za kina kuhusu mapato ya ndani ya halmashauri, ikiwamo namna minada inavyoendeshwa, fedha zinazokusanywa na matumizi yake.
Jedwali la utatuzi wa kero kila mwezi
Mbali na sakata la fedha, Dk Nchemba ameelekeza kuanzishwa kwa mfumo wa ufuatiliaji wa utatuzi wa kero za wananchi, akisema kila mwezi kutakuwa na jedwali litakaloonesha ni kero zipi zimetatuliwa na zipi zimepelekwa ngazi za juu.
“Kwa wale wanaodhani huu ni moto wa ziara, sasa hivi litakuja jedwali ambalo litaonesha kila mtu ametatua kero za wananchi gani kwenye eneo lake kila mwezi. Kila mwezi utaeleza umetatua kero gani na zipi umezipandisha ngazi ya juu kwa utatuzi,” amesema.
Dk Nchemba ameonesha kukerwa na tabia ya watumishi wa umma kuzoea matatizo ya wananchi na kuyaona kama jambo la kawaida, huku baadhi ya wananchi wakilazimika kufanya kazi za Serikali kwa niaba ya watumishi waliopo ofisini.
“Haiwezekani wananchi wawe wanafanya mambo ya Serikali na watumishi wa umma wapo. Tunataka ofisi za umma zitatue kero za watu, walioko ofisini wasizoee matatizo ya watu na kuona kama jambo la kawaida,” amesema.
Ili kuongeza uwajibikaji, Waziri Mkuu amewataka wananchi wanaofika katika ofisi za umma kuandika majina yao na malalamiko yao kwenye kitabu maalumu, na iwapo watafukuzwa au kupuuzwa, wapande ngazi za juu na kuwasilisha taarifa hizo.
“Kuanzia sasa mwananchi ukienda kwenye ofisi ya umma usiondoke bila kuandika jina lako kwenye kitabu na uandike shida yako. Wakikufukuza, fika ngazi ya juu uelezee na hicho ili tuweze kushikishana adabu,” amesema.
Katika mkutano huo wakazi wa Kiteto walipata fursa ya kuwalisha kero zao mbalimbali mbele ya waziri mkuu ambaye alitoa maelekezo kwa viongozi kutafuta ufumbuzi wa kila kero iliyowasilishwa.