Hizi ndizo barabara utakapopita mwili wa Kardinali Pengo kutoka Hospitali ya Lugalo

Dar es Salaam. Kesho, Ijumaa Februari 27, 2026  waumini wa Kanisa Katoliki na Taifa kwa jumla watakuwa katika siku ya majonzi na tafakari, wakati wakiaga mwili wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kabla ya maziko yake yatakayofanyika katika Kituo cha Hija Pugu.

Ni siku ya kumbukizi ya maisha yaliyoacha alama si tu madhabahuni, bali pia katika mioyo ya waumini na Watanzania wengi walioguswa na sauti yake ya upatanisho, haki na maadili.

Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi, mwili wa Kardinali Pengo utachukuliwa kutoka Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, ulikohifadhiwa saa 1:30 asubuhi.

Msafara utapita katika barabara za Ali Hassan Mwinyi na Ohio kuelekea Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, ambako ibada ya kumuaga itafanyika.

Akizungumzia ratiba hiyo leo Alhamisi Februari 26, 2026, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Joseph Masenge amesema wale watakaoshindwa kufika kanisani wanashauriwa kusimama kandokando ya barabara ambazo msafara utapita ili kutoa heshima zao za mwisho.

“Tayari tumeshafanya maandalizi na Jeshi la Polisi katika barabara zote ambako mwili wa Baba Kardinali utapita kuanzia Ijumaa hadi Jumamosi.

“Siku ya Jumamosi, mwili utatolewa hapa kanisani kuelekea Pugu kupitia Barabara ya Nyerere. Wananchi wanahimizwa kusimama kandokando ya barabara hizo ili kutoa heshima zao za mwisho kwa Baba Kardinali Pengo,” amesema Padri Masenge.

Gazeti la Mwananchi limemtafuta Mkuu wa Trafiki Kanda ya Dar es Salaam, Boniphace Mbao, lakini hakupatikana.

Hata Mkuu wa Trafiki Ilala, Salum Morimori ameeleza kuwa si msemaji, huku Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipotafutwa simu yake, iliita bila kupokewa.

Akifafanua zaidi kuhusu ratiba hiyo, Padri Masenge amesema kesho kuanzia saa 1:30 asubuhi, mwili wa Kardinali Pengo utachukuliwa kutoka Hospitali ya Lugalo kuelekea Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph.

Amesema utapokewa na Askofu Mkuu, Jude Thadaeus Ruwa’ichi na kusali sala kwenye mlango wa kanisa kisha kuingizwa kanisani na watu kuruhusiwa kutoa heshima za mwisho hadi saa 9:30 alasiri.

“Saa 10:00 jioni Misa itaanza baada ya hapo watu wataendelea kusali  na kutoa heshima za mwisho hadi Jumamosi asubuhi saa 12, mwili utachukuliwa Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph na kupelekwa Pugu ambapo watu wataendelea kutoa heshima za mwisho hadi saa 3:30 asubuhi,” amesema.

Pia, amesema Misa itaanza saa 4:00 asubuhi baada ya hapo utaratibu wa mazishi utaendelea akiwaomba waumini na Taifa kuendelea kumuombea Kardinali Pengo.

Gazeti la Mwananchi imefika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph  na kukuta maandalizi kwa ajili ya tukio la kumuaga mwili wa Kardinali Pengo yakiendelea, huku waumini mbalimbali wakiendelea kusaini kitabu cha maombolezo, akiwamo James Mbatia.

Wananchi walipanga foleni wakisubiri kusaini kitabu cha maombolezo, huku baadhi ya viongozi wakiingia ofisini kumpa pole Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, Ruwa’ichi.

Katika maandalizi hayo, pia umewekwa utaratibu wa waumini kufuatilia ibada hiyo kupitia runinga zitakazofungwa nje kwa wale watakaoshindwa kupata nafasi ya kuingia kanisani.

Sababu maaskofu kuzikwa kanisani

Mwili wa Kardinali Pengo utazikwa ndani ya kanisa kunakofanyika Misa za Hija katika Kituo cha Hija Pugu, ambacho yeye ndiye muasisi na alikizindua mwaka 1995.

Askofu Msaidizi mstaafu, Methodius Kilaini amesema Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph ndilo kanisa la Askofu.

Amesema kama Kardinali Pengo asingekuwa na wosia wa kuzikwa Pugu, basi angezikwa ndani ya kanisa hilo.

“Yapo makaburi ya maaskofu wengine mle ndani, walipozikwa yakasawazishwa na kuwa flati, juu yake kuna maandiko tu japo siku hizi mengi hayawi flati yanakuwa na kitu juu na kuwa makaburi kama yalivyo makaburi mengine,” amesema.

Akifafanua sababu za maaskofu kuzikwa ndani ya kanisa amesema ni kutokana na mshikamano waliouweka na kanisa.

“Ni kama wamefunga ndoa na kanisa, ndiyo sababu wanavalishwa pete ambayo hiyo ni kama mshikamano au ishara kwamba wamefunga ndoa na kanisa,” amesema Askofu Kilaini.

Amesema makanisa ya zamani likiwamo la Mtakatifu  Joseph, ili kuzika wanachimba upya kisha baada ya mazishi wanajengea, tofauti na makanisa mapya ambayo yanajengwa hivi sasa.

“Mfano ni lile la Mwanza ambalo lilijengwa na Baba Askofu Ruwa’ichi, lile lina makabuli 16, hata hili la kwetu Bukoba (Kagera) lina makabuli matatu yako ‘spea’ pale,” amesema.