Video: Polisi Kuhusu Mwenyekiti BAVICHA Kupotea – ”Amekimbia Kesi ya Mauaji”

Bakari Mahundu
February 26, 2026
0 Comments

Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limetoa ufafanuzi rasmi kufuatia taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa watuhumiwa wanne, akiwemo Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) Mkoa wa Iringa, Ibrahimu Myovella, wamepotea wakiwa mikononi mwa polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi, amesema madai hayo si ya kweli na hayana msingi wowote.

Kamanda Bukumbi amewataja watu waliodaiwa kupotea kuwa ni Ibrahimu Myovella (33), Asajile Anthony (33), Anthony Mwasika (29) pamoja na Ally Kalolo (26), akibainisha kuwa wote ni watuhumiwa katika tukio la mauaji na walifanikiwa kutoroka wakati polisi wakiendelea na taratibu za kuwakamata.

Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi halijawahi kuwakamata watuhumiwa hao, bali linaendelea na juhudi za kuwasaka ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limewahakikishia wananchi kuwa litaendelea kutoa taarifa rasmi kuhusu hatua za uchunguzi, huku likiwataka wananchi kupuuza taarifa zisizo sahihi zinazoweza kusababisha taharuki na sintofahamu katika jamii.