Aliyekuwa Anawauza Wakenya Kujiunga Na Jeshi Urusi Akamatwa

Bakari Mahundu
February 26, 2026
0 Comments

Idara ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) nchini Kenya imemkamata mshukiwa mmoja anayedaiwa kuhusika katika mtandao wa kuwarubuni raia kujiunga na jeshi la Urusi kupitia ahadi za kazi bandia nje ya nchi, tukio linaloibua hofu mpya kuhusu biashara haramu ya binadamu inayovuka mipaka ya mataifa.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa Jumatano, Februari 25, DCI ilisema mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 33 alikamatwa katika mji wa mpakani wa Moyale baada ya kufuatiliwa kwa muda na vyombo vya usalama. Maafisa wanasema alikua akiwalenga watu walio katika mazingira magumu kiuchumi na kijamii, akiwashawishi kwa ahadi za ajira katika mataifa ya Ulaya kabla ya kuwaelekeza safari kuelekea Urusi, ambako walidaiwa kuishia kuingizwa katika shughuli hatari.

Mshukiwa huyo, Festus Omwamba, anaaminika kuwa sehemu ya mtandao mpana wa uhalifu unaohusisha usafirishaji haramu wa watu. Baada ya kukamatwa, alisafirishwa hadi makao makuu ya DCI kwa ajili ya mahojiano zaidi huku akitarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Kwa mujibu wa DCI, waathiriwa wengi walikuwa wanadanganywa kwa kuahidiwa kazi halali zenye mishahara mikubwa, lakini walipofika walijikuta wakilazimishwa kushiriki kazi zisizo halali na zenye hatari kubwa, hali inayokiuka haki za binadamu na kuhatarisha maisha yao. Maafisa wa uchunguzi wanasema mbinu zinazotumiwa na mitandao hiyo ni pamoja na kutumia mawakala wa ndani, nyaraka bandia na njia zisizo rasmi za kusafiri.

Ripoti iliyowasilishwa mbele ya Bunge la Taifa la Kenya inaonyesha kuwa takribani Wakenya 1,000 wamewahi kushawishiwa kwa njia kama hizo kujiunga na vikosi vya Urusi au kazi zinazohusishwa na maeneo ya migogoro, jambo linaloongeza wasiwasi kuhusu usalama wa raia wanaotafuta ajira nje ya nchi.

DCI imewahakikishia wananchi kuwa inaendelea kushirikiana na mashirika mengine ya usalama ya ndani na kimataifa ili kuwabaini washirika wote wa mtandao huo na kuwachukulia hatua kali za kisheria. Aidha, imeonya umma kuwa makini na matangazo ya ajira yasiyo rasmi na kuripoti mara moja watu au taasisi zinazotilia shaka ili kuzuia visa vingine vya udanganyifu na usafirishaji haramu wa binadamu.