Uwekezaji wa Anga na Reli Waongeza Maradufu Uwezo wa Usafirishaji Mizigo

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa,akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar  Es Salaam leo Februari 26, 2026.

SERIKALI imesema kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya usafiri wa anga na reli umeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa ubebaji wa mizigo nchini, huku kila sekta ikiwa na nafasi na mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati akifafanua mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Februari 26, 2026 kuhusu usafiri wa anga, Msigwa amesema kuwa uwekezaji uliofanywa kupitia Kampuni ya Ndege Tanzania, Air Tanzania Company Limited, umeongeza kwa kasi uwezo wa kubeba mizigo ya kimataifa na kikanda.

Ameeleza kuwa ununuzi wa ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300F pamoja na upanuzi wa safari za kimataifa umewezesha kuongezeka kwa mizigo kutoka tani 2,567 mwaka 2021/22 hadi tani 6,919 mwaka 2024/25.

“Ongezeko hili limechangiwa na upanuzi wa safari za kimataifa, hali iliyorahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, mbogamboga na matunda kwenda masoko ya nje kwa haraka zaidi,” amesema Msigwa, akibainisha kuwa usafiri wa anga una faida ya kasi na unafuu kwa mizigo inayohitaji kuwahi sokoni au inayoharibika haraka.

Kwa upande wa reli, Msigwa amesema kuwa uwekezaji kupitia Shirika la Reli Tanzania umeongeza uwezo mkubwa wa kubeba mizigo kwa wingi na kwa gharama nafuu zaidi. Tangu kuanza kwa huduma za Reli ya Kisasa (SGR), zaidi ya tani 52,305 za mizigo zimesafirishwa hadi Desemba 2025, huku maboresho ya reli ya zamani (MGR) yakiongeza uwezo wa kubeba mizigo mizito kwa kuongeza kiwango cha ekseli kutoka tani 13.5 hadi 18.5.

Amefafanua kuwa tofauti na ATCL inayolenga zaidi mizigo ya thamani kubwa au inayohitaji kufikishwa kwa haraka, reli inalenga mizigo mikubwa na mizito kama saruji, makaa ya mawe, nafaka na bidhaa za viwandani, hususan katika safari za ndani na nchi jirani.

Hata hivyo, Msigwa amesisitiza kuwa sekta hizo mbili zinakamilishana badala ya kushindana.

“ATCL na TRC zinafanya kazi kwa mfumo unaosaidiana. Ndege zinasaidia kufungua masoko ya mbali kwa haraka, wakati reli inahakikisha mizigo inasafirishwa kwa wingi kutoka uzalishaji hadi bandarini au nchi jirani kwa gharama nafuu,” amesema.

Kwa mujibu wa Serikali, wakati ATCL imeongeza mapato ya fedha za kigeni kupitia safari za kimataifa, TRC imeimarisha mnyororo wa thamani wa ndani kwa kuunganisha maeneo ya uzalishaji na bandari, hatua inayochochea biashara ya kikanda na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania.

Kwa ujumla, Msigwa amesema mafanikio hayo yanaakisi mkakati wa Serikali wa kujenga mfumo jumuishi wa usafiri unaounganisha anga, reli na bandari, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa ubebaji wa mizigo, kupunguza gharama za usafirishaji na kukuza uchumi wa taifa.