Mbozi. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na ushindi katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Shiwinga Jimbo la Mbozi mkoani Songwe, baada ya mgombea wake, Menard Mzumbwe kupata kura 5,030 kati ya kura halali 5,210 zilizopigwa.
Uchaguzi huo umefanyika leo Alhamisi, Februari 26, 2026.
Akitangaza matokeo rasmi msimamizi wa uchaguzi wa Kata ya Shiwinga, Selestin Luambano, amesema jumla ya wapigakura walioandikishwa walikuwa 6,852, huku 5,229 wakijitokeza kupiga kura.
Kati ya kura hizo, halali zilikuwa 5,210 na kura 19 zilikataliwa.
Luambano akitangaza matokeo hayo amesema Mzumbwe (CCM) amepata kura 5,030 huku mgombea Matias Dulle wa Chama cha ADC Wazalendo amepata kura 62, Elly Shitindi wa Ada-Tadea amepata kura nane, Mary Daud (UPDP) kura 15, Neema Abadallah (UMD) kura 22, Emily Siwale (SAU) kura 24, Mussa Dulle (Chama-Makini) kura 32 na Cosam Mwakyusa (TLP) kura 17.
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo, mgombea wa udiwani kupitia Chama cha UPDP, Mary Daudi, ameishukuru Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) pamoja na wasimamizi wa uchaguzi kwa kusimamia mchakato huo kwa haki na uwazi kuanzia kampeni hadi siku ya kupiga kura.
Uchaguzi huo umehitimishwa kwa amani huku CCM kikiendelea kushikilia kiti hicho cha udiwani kwa ushindi mkubwa wa kura.