Grayson Msingwa: Hatutavumilia Matumizi Mabaya ya Usajili wa Meli – Video

Global Publishers
February 27, 2026
0 Comments

Msemaji wa Serikali, Grayson Msingwa

Serikali imethibitisha kuwa meli iliyokamatwa nchini El Salvador ilikuwa imesajiliwa Tanzania kupitia upande wa Zanzibar, huku ikieleza kuwa tayari hatua za kisheria na kiutawala zimechukuliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji wa Serikali, Grayson Msingwa, amesema tukio hilo lisitumike kuichafua nchi kwani meli hiyo ilikuwa inafanya shughuli zake nje ya mipaka ya Tanzania.

Msingwa, amesema usajili wa meli hufuata miongozo ya kimataifa chini ya International Maritime Organization (IMO), ambapo nchi wanachama huruhusiwa kusajili meli kupitia mawakala walioko katika maeneo mbalimbali duniani. Alifafanua kuwa usajili hauhusiani moja kwa moja na umiliki au uendeshaji wa kila siku wa meli husika.

Meli hiyo ilikamatwa na mamlaka za El Salvador kwa tuhuma za ukiukwaji wa sheria za huko na baadaye kulipishwa faini kwa mujibu wa taratibu zao hata hivyo, Serikali imesisitiza kuwa hakuna Mtanzania aliyekamatwa au kuhusishwa moja kwa moja na makosa hayo.

Katika hatua za ndani zilizochukuliwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeufuta rasmi usajili wa meli hiyo ili kuondoa hadhi ya kubeba bendera ya Tanzania. Sambamba na hilo, mamlaka zimeanzisha uchunguzi wa kina kuhusu wakala aliyesimamia usajili huo, na hatua za kinidhamu pamoja na kifedha zimeanza kutekelezwa, ikiwemo kutoza faini kwa mujibu wa masharti ya usajili endapo kutabainika ukiukwaji wa taratibu.

Msingwa amesema hatua hizo zinaonesha msimamo wa Serikali wa kutovumilia matumizi mabaya ya mfumo wa usajili wa meli.

“Tunataka kulinda heshima ya nchi na kuhakikisha bendera ya Tanzania haitumiki katika mazingira yanayoweza kuathiri taswira yetu kimataifa,” amesisitiza.

Aidha, Serikali imeanza mapitio ya mfumo mzima wa usajili wa meli kupitia mawakala ili kuimarisha udhibiti na ufuatiliaji lengo ni kuziba mianya inayoweza kuruhusu meli zisizozingatia sheria kutumia usajili wa Tanzania.