Saida; Nahodha wa Mv Ilemela aliyeigusa jamii kipekee

Mwanza. Imezoeleka masikioni mwa watu kuwa, mwanamke ni nguzo ya jamii, lakini unapomuona Saida Khailallah akiwa kwenye usukani wa kivuko katikati ya mawimbi ya Ziwa Victoria, unagundua kuwa msemo huo una maana pana zaidi.

Si nguzo tu ya jamii yake, bali ya ujasiri, uthubutu na mabadiliko ya fikra katika jamii inayojifunza kuwa uwezo haupimwi kwa jinsia.

Wakati baadhi ya wanawake na wasichana huikwepa taaluma ya ubaharia kwa kuhofia hatari za majini na umbali wa kuwa mbali na familia, Saida amechagua kuyakabili mawimbi ana kwa ana. Anakabiliana nayo kwa utulivu, umakini na kujiamini.

Kabla ya kuwa nahodha, alifanya kazi za kawaida, lakini zenye manufaa makubwa kwa jamii, akianza kuuza mafuta kwenye kituo alikojifunza uvumilivu kwa wateja na biashara.

Baadaye alihamia kwenye huduma za afya, akiwa muuguzi kwenye Kituo cha Afya Butimba, ambacho kwa sasa ni Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana.

Kazi zote zilimfundisha maadili, nidhamu, utu na uwajibikaji.

Saida, mkazi wa Mkolani, jijini Mwanza, mke na mama wa watoto watatu, kwa zaidi ya miaka 10 ameendesha vyombo vya majini katika Ziwa Victoria.

Kwa miaka mitano sasa ni nahodha wa Mv Ilemela, kivuko kinachofanya safari kati ya Kayenze, Kisiwa cha Bezi na Ukerewe.

Kwa zaidi ya saa mbili za safari ya kwenda na kurudi, hubeba abiria wasiopungua 200 wanaomtegemea kuwafikisha salama.

Cha kuvutia zaidi anapokuwa kwenye usukani haonekani kuwa na papara wala wasiwasi, bali uso uliotawaliwa na tabasamu la kujiamini linalowatuliza hata abiria wenye hofu ya mawimbi.

Saida anasema wazo la kuwa baharia halikuja kwa bahati mbaya, siku moja alimwona mwanamke akiendesha chombo cha majini na hapo ndipo alipojijengea imani kwamba naye anaweza.

“Nilimuona mdada anafanya kazi hii, akanivutia nikaenda kusoma na sasa nina uzoefu wa miaka 10 kwenye kazi hii,” anasema.

Anasema alijiunga na masomo ya ubaharia kwa miaka mitatu, akajifunza taaluma ya uendeshaji vyombo vya majini, usalama, urambazaji na uhandisi wa msingi wa mitambo.

Anasema baada ya kuhitimu alianza kazi na chombo cha Nyehunge, baadaye akafanya kazi Kigongo Feri, kabla ya kuaminiwa kuendesha Mv Ilemela, nafasi aliyoishika kwa miaka mitano sasa.

Ujuzi wake katika urambazaji unamwezesha kujua mwelekeo sahihi kwa kutumia compas, GPS na ramani za majini, kuelewa mikondo ya maji, hali ya hewa na mawimbi.

Japokuwa ni taaluma inayohitaji usahihi wa hali ya juu, Saida anaiendesha kwa tabasamu na utulivu.

Ni zaidi ya kushika usukani

Wapo wanaodhani kazi ya nahodha ni kushika tu usukani na kuongoza chombo.

Lakini Saida anaeleza ubaharia ni zaidi ya hapo, kwa kuwa anahakikisha mizigo inayopakiwa haizidi uwezo wa chombo, akisimamia kwa makini upangaji na uzito wake.

“Usalama wa abiria ni jukumu langu, lazima nijiridhishe kila kitu kiko sawa kabla ya kuondoka na wakati wa kushusha nasimamia,” anasema.

Kwa uzoefu wake, hata sauti ya injini ni lugha anayoielewa, akieleza akisikia mlio wa injini anajua kama kuna shida au ipo sawa kwa ajili ya kuendelea na safari.

Ujuzi huo haumfanyi tu nahodha, bali pia mlezi wa chombo anachokiendesha.

“Nikisikia tu sauti ya injini najua kama ipo sawa au inahitaji kufanyiwa marekebisho,” anasema.

Kama ilivyo katika maeneo mengine, changamoto hazikosekani. Kwa Saida nyavu za wavuvi zinazotegwa kwenye njia ya feri ni tatizo la mara kwa mara akieleza zikinasa kwenye propela, chombo hushindwa kwenda kwa kasi inayotakiwa.

“Tukikumbana na hali hiyo, kuna mtu huingia majini kukata nyavu ili tuendelee na safari. Changamoto hii tunakutana nayo mara nyingi ila tunazikwepa kwa sababu wavuvi wanaweka madumu, ukiona hayo unapita katikati kukwepa nyavu,” anafafanua.

Mawimbi makubwa nayo ni mtihani mwingine, “wimbi baya zaidi ni la pembeni, ukikosea kulikabili linaweza kuleta madhara …kwa hiyo ukikutana na wimbi lazima ulifuate linapotokea la sivyo watu wataumia.”

Anasema changamoto nyingine ni ukungu mzito unaofunika ziwa, hivyo hulazimika kutumia compas na GPS kwa kuwa macho hayawezi kuona mbele.

Kwa nini wanawake wachache?

Swali linabaki kwa nini bado baadhi ya wanawake wanaikwepa taaluma ya ubaharia?

Wengi huogopa hatari za maji, simulizi za ajali au kuamini kuwa kazi hiyo inahitaji nguvu.

 Pia, wapo wengine huona changamoto ya kukaa mbali na familia kwa muda mrefu.

Lakini kwa Saida vizingiti hivyo vinaweza kuvukwa kwa mafunzo, nidhamu na kujiamini akieleza:

“Hakuna kazi ya mwanamume au mwanamke …kazi ni taaluma na taaluma inahitaji kujifunza na kufanya kwa bidii.”

Anawahamasisha wasichana kusomea ubaharia, akisisitiza kuwa lazima wawe tayari kufanya kazi zote ikiwa ni pamoja na kupiga mbizi pale inapohitajika, kufunga mizigo na kushughulikia dharura.

Kwa abiria wengi, kumuona Saida kwenye usukani si jambo la kawaida bali ni tukio linalowatia moyo na kuwapa simulizi mpya ya matumaini.

Kila safari ya Mv Ilemela si tu mwendo kutoka Kayenze hadi Ukerewe, ni safari ya fikra za jamii, kutoka kwenye dhana potofu hadi kwenye uhalisia wa uwezo wa mwanamke.

Vilevile, ni safari ya msichana mwenye ndoto mpya na mzazi anayepata ujasiri wa kusomesha binti yake bila mipaka ya fikra.

Jackline Gusonwa, mkazi wa Kisiwa cha Bezi, anasema mara ya kwanza kumuona Saida alipata msisimko wa kipekee na kujiapiza atahakikisha binti yake anasoma na kuwa kama nahodha huyo au zaidi.

“Nilisimama nje nikimtazama, nilikuwa natabasamu peke yangu. Nilijiambia mwanangu akiwa kama huyu dada itakuwa fahari kubwa,” anasema na kuonesha kuwa, Saida ni mfano halisi wa ndoto zinazowezekana.

Fikiri Roghert anakiri kuvutiwa akieleza: “Tunasikia hadithi nyingi za hatari za ziwani, lakini kumuona huyu mama anaendesha kwa utulivu na kujiamini kunakupa amani. Nilijisemea kweli wanawake wanaweza.”

Abiria mwingine, Neema Paul anasema kila anaposafiri na Mv Ilemela hujihisi salama zaidi akimuona Saida kwa kuwa anaamini mwanamke akiamua kufanya jambo hulifanya kwa moyo wake wote.

“Unamuona alivyo makini, anatoa maelekezo kwa abiria kwa sauti ya utulivu (anamuangalia Saida akimuelekeza mmoja wa abiria mwenye gari la mzigo namna ya kulitoa salama katika kivuko hicho). Hata picha nilishawahi kupiga naye mara ya kwanza nilivyomuona,” anasema.

Hamis Baraka, mfanyabiashara wa samaki anayesafiri mara kwa mara kati ya Kayenze na Ukerewe anasema uwepo wa Saida umebadili mtazamo wake.

“Zamani nilidhani kazi hizi ni za wanaume pekee maana tangu utoto hadi nimekua nikisikia mabaharia ni wanaume. Lakini sasa naona mwanamke anaweza na anaweza vizuri zaidi,” anasema.

Saida anakiri kuwa abiria wengi hupenda kupiga naye picha pindi tu wanapomuona.

Anaeleza kwenye jamii inayomzunguka hakutani na changamoto ya ubaguzi zaidi ya kuwa motisha kwenye jamii yake.