Yajue mambo yanayoharibu saumu | Mwananchi

Dar es Salaam. Katika Makala iliyopita tuliangazia sababu zinazoruhusu mtu Kisharia kufungua mchana wa Mwezi wa Ramadhani, ambapo tulibainisha sababu tatu, ambazo ni kusafri safari ya halali, ukongwe na kuumwa. Makala hii ni mwendelezo…

Mwanamke mwenye hedhi au nifasi ni haramu kwake kufunga. Na akifunga saumu yake si sahihi. Mtume (Rehema na amani zimshukie) amesema: “…Je, si kweli kwamba anapopata hedhi haswali wala hafungi? Huo ndiyo upungufu wa dini yake…” Mwanamke huyu atalazimika kulipa siku alizofungua. Aisha (Allah Amridhie) amesema:

Tulikuwa tukipata hedhi katika zama za Mtume wa Allah, tukaamrishwa kulipa saumu wala hatukuamrishwa kulipa Swala.” Ikiwa damu itaanza kutoka hali ya kuwa mwanamke amefunga, hata kama ni muda mfupi kabla ya kuzama jua, saumu yake ya siku hiyo itabatilika na atalazimika kuilipa.

Na ikiwa atatwaharika katikati ya mchana wa Ramadhani, saumu ya siku hiyo haitahesabika, kwa kuwa mwanzo wa siku ulikuwa na hali inayopingana na saumu.  Lakini akitwaharika usiku wa Ramadhani, hata kama ni muda mfupi kabla ya alfajiri, atalazimika kufunga siku inayofuata. Hata kama asubuhi akiamka na hajaoga josho la Kisharia, saumu yake ni sahihi kwa mujibu wa kauli yenye nguvu ya wanazuoni.

Mwanamke akiwa mjamzito au ananyonyesha, na akaogopa madhara kwa nafsi yake anaruhusiwa kufungua na kuilipa siku hiyo bila ya fidia yoyote. Na ikiwa ataogopa kufunga kwa ajili ya mtoto wake tu (na sio nafsi yake), basi pamoja na kulipa siku hiyo, pia atalazimika kutoa fidia kwa mujibu wa kauli sahihi ya wanazuoni.  Na fidia yenyewe ni kiasi cha robo pishi (takribani gramu 562 au nusu na robo). Mtume wa Allah amesema: Hakika  Allah amempunguzia msafiri nusu ya Swala na (amemruhusu kufungua) saumu; na pia amempunguzia mjamzito na mwenye kunyonyesha saumu..”

Saumu maana yake ni kujizuia kwa nia kutokana na vitu vinavyoharibu saumu, kuanzia kuchomoza alfajiri hadi kuzama jua. Na miongoni mwa mambo yanayoharibu Saumu. Mosi, Kujamiana mke na mume  mchana wa Ramadhani hali ya kuwa wamefunga kwa makusudi, saumu zao hubatilika, na wanatakiwa kutubu na kuomba msamaha, kulipa siku waliyojamiiana na kutoa kafara, kafara lenyewe ni  kuacha huru mtumwa, kama hana, basi afunge miezi miwili mfululizo, asipoweza kufunga miezi miwili mfululizo, alishe maskini sitini, kila mmoja apewe kiasi cha robo pishi (takribani gramu 562 au nusu na robo) cha chakula bora au chakula cha kawaida kinachotumika katika nchi yake.

Hairuhusiwi kuhamia kwenye kulisha maskini isipokuwa kama hawezi kufunga kwa udhuru halali, kama ugonjwa au hofu ya kupata madhara.  Ni lazima miezi miwili iwe mfululizo. Hairuhusiwi kukatisha isipokuwa kwa udhuru wa kisharia kama siku za Idd, siku za Tashriq, hedhi au nifasi kwa mwanamke. Akikatisha bila udhuru hata siku moja tu, atalazimika kuanza upya ili kukamilisha mfululizo uliotajwa.

Pili: Kutokwa na manii (mbegu za uzazi) kwa hiari. ikiwa mwenye kufunga atatokwa na manii kwa hiari yake, kwa njia ya kubusu, kugusa, kufanya punyeto, au kwa njia nyingine yoyote, saumu yake hubatilika na atalazimika kulipa siku hiyo tu. Ama akibusu au kugusa bila kutokwa na manii, hafungui. Ama kutokwa na manii kwa ndoto (usingizini mchana wa Ramadhani) au kwa mawazo tu bila tendo la kimwili, hakufunguzi saumu.

Tatu: Kula au kunywa kwa  kufikisha chakula au kinywaji tumboni kupitia mdomoni au puani, bila kujali aina ya chakula au kinywaji. Kadhalika, kila kitu chenye maana ya kula na kunywa kina hukumu hiyo hiyo.

Mfano wa kutiwa damu mwilini kwa njia ya sindano kiasi kwamba mtu anajitosheleza nayo badala ya kula na kunywa. Vilevile, Sindano za lishe (drips) zinazochukua nafasi ya chakula na kinywaji. . Ama sindano zisizo za lishe, hazifunguzi saumu, maadamu hazifikii tumboni kama ilivyotajwa.

Nne: Kupiga chuku au kuumika (Hijama)Hiki ni kitendo cha kukata sehemu ya juu ya ngozi kwa makusudi ili kutoa damu mwilini, bila kukata mishipa mikubwa. Mtume wa Allah amesema: Amefungua mwenye kupiga chuku na anyefanyiwa chuku.

Hivyo, hairuhusiwi kwa mwenye kufunga saumu ya wajibu kutoa damu yake kwa hiari (kwa mfano kuchangia damu), isipokuwa katika hali ya dharura kubwa, kwa sharti asidhurike. Na atafungua siku hiyo kisha ailipe. Ama damu inayotoka bila kukusudia, kama vile kutokwa na damu ya puani, damu ya jeraha, kung’olewa jino, n.k. Hayo hayafunguzi saumu

Tano: Kujitapisha kwa makusudi ni kutoa kilichomo tumboni, chakula au kinywaji, kupitia mdomoni kwa hiari. Mtu akitapika kwa makusudi hufungua swaumu na anawajibika kulipa siku hiyo. Ama ikiwa kutapika kumemtoka bila hiari yake, basi hilo halibatilishi swaumu yake. Sita: Mwanamke akiona damu ya hedhi au ya nifasi, swaumu yake hubatilika, iwe ameiona mwanzoni mwa siku au mwishoni mwa siku. 0712 69081