Pedro, Barker jeuri ipo hapa

IMEBAKI muda usiozidi saa 48 kabla ya Dabi ya Kariakoo haijapigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, huku makocha wa Yanga na Simba kila mmoja ni kama ana jeuri ya kujivuni jeshi lake katika kumpa furaha huko Zanzibar.

Achana na matokeo ya suluhu iliyopata Simba juzi Jumatano mbele ya Dodoma Jiji inayoonekana kama imeishusha morali, lakini soka ililopiga kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, limebeba matumaini mapya kwa Wanamsimbazi.

Matumaini hayo kwa Wanamsimbazi, wenzao wa Jangwani wanayo tena kwa kiwango kikubwa baada ya hiyo juzi kuishushia mvua ya mabao JKT Tanzania ilipoichapa 5-0 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Kama ulifuatilia mechi za watani hao wa jadi zilizochezwa juzi Jumatano, kuna kitu utakuwa umekigundua kutokana na vikosi vilivyopangwa vikionyesha ndio vile vya kazi vinavyoaminiwa na mabenchi ya ufundi ya timu hizo.

Yanga inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuifunga Simba mechi sita mfululizo za mashindano tofauti.

Mara ya mwisho Simba kuifunga Yanga ilikuwa katika Ngao ya Jamii iliyochezwa Agosti 13, 2023 kwa penalti 3-1, baada ya hapo, Yanga imetembeza vipigo vinne katika Ligi na viwili Ngao ya Jamii.

Ubabe wa Yanga kwa Simba katika Ligi Kuu Bara matokeo yalikuwa hivi; Simba 1-5 Yanga (Novemba 5, 2023), Yanga 2-1 Simba (Aprili 20, 2024), Simba 0-1 Yanga (Oktoba 19, 2024) na Yanga 2-0 Simba (Juni 25, 2025). Pia mechi mbili za Ngao ya Jamii matokeo yalikuwa hivi; Yanga 1-0 Simba na Yanga 1-0 Simba.

DAB 04


Kupitia usajili wa dirisha dogo uliofunguliwa Januari 1, 2026 na kufungwa Januari 30, 2026, Yanga na Simba kila moja imeingiza maingizo mapya ili kuboresha maeneo yaliyoonekana kuhitaji nguvu.

Yanga imeingiza mashine sita katika dirisha dogo, nyota ambao wanakwenda kucheza Dabi ya Kariakoo ya kwanza baada ya kukosekana Ngao ya Jamii.

Nyota hao ni kipa Hussein Masalanga, kiungo mkabaji Mohamed Damaro, viungo mshambuliaji Allan Okello na Buba Jammeh, pia washambuliaji wawili Emmanuel Mwanengo na Laurindo Aurelio ‘Depu’. Pia kupitia dirisha dogo imemrudisha beki wa kulia, Yao Kouassi baada ya kupona majeraha ya goti na ameshakiwasha.

Kati ya nyota hao, tayari tumeona Depu akionyesha makali kwa kufunga mabao matano katika mechi nne za ligi akiwa na asisti moja, hivyo kumfanya kuwa na mchango wa mabao matano.

Ni kiwango kizuri ameanza nacho mshambuliaji huyo, huku pale eneo la kati, Damaro naye akiweka utawala. Kumbuka Damaro amekabidhiwa mechi hii iliyopewa jina la Damaro Day.

Okello ni kama anajitafuta, licha ya kuaminiwa kwa kucheza mfululizo, lakini bado hajageuza nafasi kuwa bao kitu ambacho hata kocha mkuu wa kikosi hicho, Pedro Goncalves kusema anahitaji kuongeza umakini licha ya kwamba anafurahishwa na kiwango chake sambamba na nyota wengine wa Yanga.

Kwa sasa ukikiangalia kikosi cha Yanga, unaweza kuvipanga viwili kisha kila kimoja kikacheza mechi yoyote ya mashindano na kukupa matokeo mazuri.

Kama kocha Pedro Goncalves ataamua kuanza na mziki mnene, basi ni wazi atayapanga majeshi yake namna hii; Langoni atasimama Djigui Diarra, huku mabeki wa pembeni watakuwa Israel Mwenda na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ilihali wale wa kati watakuwa ni; Dickson Job na Ibrahim Bacca.

DAB 02


Viungo atawajaza kina Mohamed Damaro, Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Pacome Zouzoua na Allan Okello, kisha mshambuliaji akisimama Laurindo Depu.

Kikosi kingine kina muonekano huu; Aboutwalib Mshery, Yao Kouassi, Chadrack Boka, Frank Assinki, Bakari Mwamnyeto, Aziz Andabwile, Edmund John, Mudathir Yahya, Prince Dube, Lassine Kouma na Buba Jammeh.

Hapo kumbuka kuna vifaa vingine vitakuwa vinasubiri nje akiwamo kipa Hussein Masalanga, Kibwana Shomary, Abubakar Nizar ‘Ninju’, Abdulnassir Mohamed ‘Casemiro’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Farid Mussa, Shekhan Ibrahim, Emmanuel Mwanengo na Clement Mzize aliye majeruhi.

DAB 03


Kati ya timu ambazo zimefanya usajili wa nyota wengi kupitia dirisha dogo ni Simba, hiyo imetokana na changamoto mbalimbali ndani ya kikosi hicho ikiwamo majeruhi ya wachezaji muhimu, huku pia ikipokea ofa za kuwauza Steven Mukwala, Kibu Denis na Jean Charles Ahoua.

Wachezaji nane wapya waliotua Simba dirisha dogo ni Djibril Kassali, Libasse Gueye, Ismael Olivier Toure, Clatous Chama, Nickson Kibabage, Inno Loemba, Baraka Mwangosi na Anicet Oura, ambao ukimuweka kando Mwangosi, waliobaki wote wameingia kikosi cha kwanza.

Juzi katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji, wachezaji saba wapya kati ya nane walianza, huku wale waliokuwepo tangu msimu unaanza wakiwa wanne ambao ni Shomari Kapombe, Rushine De Reuck, Yusuph Kagoma na Seleman Mwalimu.

Steve Barker ambaye ni kocha wa Simba, hakubadili kikosi kutoka kile kilichoifunga Tanzania Prisons mabao 2-0, hivyo unaweza kusema hilo ndilo jeshi lake la maangamizi.

Kikosi cha kwanza cha Simba kipo hivi; kipa Djibril Kassali, mabeki wa pembeni Shomari Kapombe na Nickson Kibabage. Mabeki wa kati Rushine De Reuck na Ismael Toure. Viungo kuna Yusuph Kagoma, Libase Gueye, Inno Loemba, Clatous Chama na Anicet Oura, kule mbele anasimama Seleman Mwalimu.

DAB 01


Kikosi kingine cha Simba kipo hivi; Hussein Abel, David Kameta, Anthony Mligo, Vedastus Masinde, Naby Camara, Allasane Kante, Morice Abraham, Semfuko Charles, Jonathan Sowah, Elie Mpanzu na Neo Maema.

Waliopo nje ni Kipa Yakoub Suleiman (majeruhi), mabeki Wilson Nangu (majeruhi), Abdulrazack Hamza (majeruhi), kiungo mshambuliaji Ladack Chasambi na mshambuliaji Baraka Mwangosi.

Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker amesema: “Tulihitaji kushinda (dhidi ya Dodoma), lakini kwa bahati mbaya haijawa hivyo. Nimeridhishwa na kiwango cha wachezaji, tumetengeneza nafasi nyingi na kama tukiendelea hivi inatoa matumaini ya ushindi. Hii imeshapita, sasa tunaangalia mechi kubwa ijayo Jumapili.

“Kila mechi ina presha, hatuchezi kwa ajili ya kupambania pointi sita dhidi ya Yanga, bali ni pointi tatu kama tukicheza na timu nyingine, kiukweli tunahitaji kushinda Dabi.

“Itakuwa mechi ngumu, Yanga ina timu nzuri na sisi pia tuna timu nzuri, ni mechi kubwa hapa nchini na Afrika kwa ujumla, matumaini yetu ni kwamba watu watafurahia mchezo,”

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema: “Ni mechi nzuri (dhidi ya Simba), kila mmoja anaisubiri, ni muda mrefu wameisubiri, lakini tumepata motisha kwa kukaa kileleni.

“Kilichopo ni kufikiria namna ya kiwango cha timu, mpaka sasa tunaendelea vizuri hata mabeki wetu wanajipanga vizuri kuzuia mashambulizi, ninafurahi sana.

“Tangu nilipofika hapa, nahisi kwamba Wananchi hutuunga mkono kila wakati hapa. Tunapotoka nje ya Dar, tunapokuwa Zanzibar, ni vizuri sana. Wao ni mchezaji wa 12 na asante sana kwa ajili yao.”