Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
TAASISI kilele ya sekta binafsi inayoshughulika na tasnia ya horticulture nchini TAHA, imewasilisha rasmi mpango wa kuandaa maonesho makubwa zaidi katika historia ya sekta ya horticulture nchini — HORTILOGISTICA AFRICA 2026 — mbele ya Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo (Mb), na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo (Mb). Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Makatibu Wakuu pamoja na wajumbe wa menejimenti kutoka wizara hizo mbili.
Akiwasilisha mpango mkakati wa maandalizi ya maonesho hayo jijini Dodoma Alhamisi, Afisa Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt Jacqueline Mkindi, alisema tukio hilo la kimataifa linatarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mwezi Novemba 2026, likiwa na lengo la kufungua ukurasa mpya wa maendeleo ya sekta ya horticulture nchini na barani Afrika kwa ujumla.
“Mbali na manufaa mengine, maonesho haya yatafungua fursa pana za uwekezaji, kupanua masoko ya ndani na nje ya nchi, kuvutia watalii wa kibiashara, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi,” Dkt Mkindi aliwaeleza mawaziri hao.
Aliongeza kuwa HORTILOGISTICA AFRICA 2026 itakuwa jukwaa mahsusi la kuwaunganisha wadau wa sekta hiyo wakiwemo wazalishaji, wasafirishaji, watoa huduma za teknolojia, taasisi za kifedha na wanunuzi wa kimataifa, kwa lengo la kuongeza tija, ubora na ushindani wa mazao ya Tanzania katika soko la dunia.
Katika kikao hicho, Waziri wa Kilimo, Bw Chongolo, alisisitiza dhamira ya Serikali kuendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi ili kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na kuinua ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Kwa upande wake, Prof Mkumbo alisema maonesho hayo yanaendana kikamilifu na dira ya taifa ya kuvutia uwekezaji zaidi, kuzalisha ajira kwa Watanzania na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kwa mujibu wa TAHA, HORTILOGISTICA AFRICA 2026 si maonesho ya kawaida ya biashara, bali ni jukwaa la kimkakati litakalounganisha wadau, teknolojia, masoko na mitaji kwa lengo la kukuza maendeleo endelevu ya sekta ya horticulture nchini.
