Baraza la ardhi lafuta kesi ya ardhi kutokana na dosari za kisheria

Moshi. Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Moshi limefuta shauri la ardhi linalowahusisha wanaukoo baada ya kubaini kuwa mleta maombi alikiuka amri ya awali ya marekebisho ya hati ya maombi.

Uamuzi huo umetolewa Februari 24, 2026 na Mwenyekiti wa baraza hilo, Hussen Lukeha  baada ya kukubaliana na pingamizi la awali lililowasilishwa na mjibu maombi.

Shauri hilo la maombi namba 83/2025 lilifunguliwa na Chemli Mallya ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Sisamaro, Kata ya Kibosho Okaoni,Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro,mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 10.

Mjibu maombi katika shauri hilo ni Anna Midimito, mjane wa marehemu Mathias Mallya aliyefariki mwaka 2010, ambaye alikuwa mdogo wa mleta maombi, Chemli Mallya.

Akitoa uamuzi huo, mwenyekiti huyo amesema amepitia amri ya baraza hilo ya Novemba 24,2025 na hati ya maombi iliyorekebishwa na hati ya maombi ya awali,  anakubaliana na hoja za wakili wa mjibu maombi kuwa mleta maomi amekiuka amri ya baraza iliyomuelekeza kurekebisha aya inayofafanua ardhi yenye mgogoro tu.

“Alirekebisha aya inayofafanua mahali na kiwanja cha mdai kisha aliendelea kurekebisha aya ya 6 (a),(vi),(vii) na (xii) na kuongeza maelekezo (facts) mapya. Pia, alirekebisha aya ya uthibitisho katika maombi haya bila ruhusa au maelekezo) ya baraza hili,”amesema.

“Kitendo hicho ambacho kilifanywa na mleta maombi kinakwenda kinyume na utekelezaji wa amri ya baraza hili ya Novemba 24, 2025 na kinafanya hati ya maombi iliyorekebishwa kutokuwa sawa kwa mujibu wa Sheria.”

Amesema kutokana na kosa hilo la kisheria,nafuu iliyopo ni kuyafuta maombi hayo kwa sababu kama itafutwa hati ya maombi iliyorekebishwa ikabaki hati ya maombi ya zamani,bado hati ya maombi ya zamani ni mbovu kwa kutofafanua ardhi yenye mgogoro kwa mujibu wa sheria.

“Hati ya shauri inapofanyiwa marekebisho,hati ya mwanzo (zamani) inakufa.Hivyo basi, pingamizi la awali limekubaliwa na maombi haya yamefutwa. Wadaawa wabebe gharama zao kwa sababu mleta maombi ni mnufaika wa msaada wa kisheria kutoka Taasisi ya Msaada wa Kisheria ya AJISO,”amehitimisha.

Awali, Novemba 24,2025, baraza hilo lilitoa amri kumtaka mleta maombi arekebishe hati ya maombi ili ionyeshe ukubwa na mipaka ya ardhi yenye mgogogo (kuonyesha majirani,mahali ilipo yaani kitongoji,kijiji,kata,wilaya na mkoa) na maeneo mengine ya hati ya maombi yabakie kama yalivyo.

Mleta maombi alifanya marekebisho na kuwasilisha hati ya maombi iliyorekebishwa kwenye baraza hilo Desemba 5,2025.

Baada ya hati ya maombi kurekebishwa,kwenye baraza hilo na upande wa mjibu maombi kupewa nakala, ndipo mjibu maombi anayewakilishwa na wakili  Vitalis Lyimo alipowasilisha pingamizi la awali.

Wakili Lyimo alieleza kuwa, mleta maombi alitekeleza amri ya baraza hilo kuhusu kurekebisha aya inayofafanua ardhi yenye mgogoro lakini aliendelea kurekebisha kwenye aya ya 6 (a) (vi), (vii), (viii) na (xii) pamoja na aya ya uthibitisho bila kupata ruhusa ya Baraza.

Wakili Lyimo alirejea kesi ya madai namba 20/2020 ya CRDB Bank PLC dhidi ya Heri Microfinance Limited ambayo Mahakama ilifuta shauri baada ya amri ya Mahakama kushindwa kutekelezwa.

Kutokana na sababu hiyo wakili huyo aliomba baraza hilo lifute maombi hayo kwa madai mleta maombi ameshidnwa kutekeleza amri ya baraza hilo.

Kwa upande wake mleta maombi alidai kwamba, alirekebisha eneo ambalo baraza hilo lilimuelekeza kurekebisha,ambalo ni kufafanua ardhi yenye mgogoro jambo ambalo alieleza kuwa alilitekeleza.