Mgogoro stendi ya daladala Buza wachukua sura mpya

Dar es Salaam. Mgogoro wa stendi ya daladala katika eneo la Buza, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, umeingia hatua mpya baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Temeke kuingilia kati na kuagiza kurejeshwa kwa huduma katika stendi zilizokuwa zikitumika awali, huku uchunguzi wa kina ukianza mara moja.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Takukuru Temeke, Holle Makungu ameiambia Mwananchi kuwa taasisi hiyo imepata malalamiko ya wananchi wa eneo hilo kuhusu usumbufu wanaoupata baada ya mabadiliko ya stendi yaliyotokana na kuanza matumizi ya stendi mpya iliyojengwa Kwamamakibonge.

Ili kuondoa usumbufu kwa wananchi na kutafuta mwafaka, Takukuru imeamuru kurejesha hali ya awali ili kuhakikisha huduma za usafiri zinaendelea bila usumbufu wakati uchunguzi ukiendelea.

“Kwa mamlaka tuliyopewa tunazishauri mamlaka zinazohusika kuruhusu kuendelea kutumika kwa taratibu za awali mpaka tutakapokamilisha uchunguzi wetu na tutashauri hatua zinazofuata kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Shughuli za biashara zikiendelea katika Stendi mpya ya Buza Kwa Mama Kibonge.



Amesisitiza kuwa, Takukuru itandelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria katika kusimamia uwajibikaji na masilahi ya umma.

Msimamo wa Takukuru umekuja ikiwa Serikali imeshatangaza kuanza rasmi matumizi ya stendi hiyo ikishikilia msimamo wa kuvunja baadhi ya vituo vya barabarani kikiwamo kile cha Kwamama Kibonge, Kwalulenge na Buza Kanisani, ambavyo imevitangaza kuwa si rasmi.

Februari 10, 2026, akihutubia Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda aliagiza watendaji kuhakikisha magari yote yanayofanya safari zake Temeke yanatumia stendi hiyo mpya bila kukatisha kwenda Buza Kanisani.

Alisisitiza kuwa maagizo ya Serikali iliyowekeza katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa umma kwa kujenga stendi hiyo ni kuona inatumika, akiwasihi viongozi wa maeneo husika kusimamia kikamilifu matumizi ya miradi hiyo iliyojengwa kwa fedha za umma.

Hata hivyo, tangu kuanza kwa utekelezaji huo, mvutano umeendelea kushuhudiwa katika maeneo hayo, magari yamekuwa yakisuasua kuishia stendi mpya, huku mengi yakiendelea kuishia

Tandika, yakiwAmo yale ya Tabata, Muhimbili, Kigamboni, Vikindu na Stesheni.

Aidha, licha ya kufungwa rasmi kwa kituo cha Kwamama Kibonge, wananchi wameendelea kufurika eneo hilo wakigombania daladala na bodaboda zinazopakia kwa kukwepana na askari wanaoimarisha doria.

Wakazi wa Kwalulenge na Buza Kanisani nao wameendelea kulalamikia hatua hiyo kuwa imeaongeza gharama na usumbufu.

Hatua hiyo ilimuibua Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam, Shifaya Anaselema akaitaka Serikali kuruhusu daladala kuendelea kwenda hadi Buza Kanisani ili kuwasaidia wakazi wa maeneo hayo kuepukana na tabu wanayoipata sasa.

“Kama ni sharti la kuingia stendi liachwe litatekelezwa lakini daladala ziruhusiwe kufika hadi Buza Kanisani ili kuwadaidia wakazi wa kule kuondokana na shida ya usafiri,”

“Kwa hali ilivyo sasa ni ngumu kwa wakazi hao kutoka kule hadi kufika stendi na wakitaka kufanya hivyo wataingia gharama nyingine labda ya kupanda bajaji au kutembea umbali mrefu,”

“Na uamuzi wa kusema daladala ziishie stendi umeleta malalamiko sana, napigiwa simu nyingi kutoka kwa watu tofauti,” alisema japo hakusikiliwa.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Buza, Mohamed Mbagalo ameiambia Mwananchi kuwa tangu kuanza kwa maagizo ya Serikali, wananchi wamekuwa wakifurika ofisi za Serikali na hata majumbani kwa viongozi wao wakitaka msaada juu ya hilo.

“Wananchi hawaoni sababu ya kusitishiwa daldala za Buza Kanisani na kufutwa kwa kituo cha Kwamama Kibonge. Wanaona walikuwa wanapata huduma karibu zaidi na makazi yao, sasa hivi ofisi zetu wanakuja kwa wingi kulalamika,” amesema.

Mbali na kero hiyo, upo pia mjadala kwenye fremu za biashara, baadhi ya wafanyabiashara wameiambia Mwananchi kuwa, upatikanaji wa fremu katika stendi mpya umekuwa changamoto, wakidai nyingi zimechukuliwa na watu wachache wenye pesa wanazipangisha kwa gharama kubwa kwa wenye uhitaji.

Serikali yashikilia msimamo

Akizungumza na Mwananchi Ijumaa Februari 27, 2026, Meya wa Manispaa ya Temeke, Uzairu Athumani, amesema uamuzi wa Kamati ya Ulinzi ni kuhakikisha stendi hiyo inatumika kikamilifu kwa kuwa imegharimu pesa nyingi.

“Sisi tunatekeleza maagizo ya Waziri Mkuu na taarifa ya ukaguzi kuhusu matumizi ya stendi hiyo iliyogharimu Sh11 bilioni, tunaendelea kusimamia kuhakikisha inatumika.

“Hawa wenzetu tutakutana nao kwenye vikao rasmi tutaeleweshana ila tumeshachukua uamzi wa kusimamia utekelezaji wa matumizi ya stendi hiyo na hatutarudi nyuma,” amesisitiza.