Songea. Mgombea ubunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Lazaro Bunungu ameshinda katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Peramiho, kwa kupata kura 69,002 kati ya kura 79,720, sawa na asilimia 87 ya kura zote zilizopigwa.
Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Peramiho, Exavery Luyagaza amesema kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa kifungu cha 105(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba 1 ya mwaka 2024 ikisomwa na pamoja na kanuni ya 58C ya kanuni za uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, amemtangaza mgombea wa CCM, Dk Lazaro Bunungu kuwa mshindi wa kiti cha ubunge, Jimbo la Peramiho.
Dk Bunungu amechukuwa nafasi hiyo baada ya kiti hicho kuwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jenista Mhagama kufariki dunia Desemba 11, 2025 jijini Dodoma.
Vyama 14 vya siasa vilisimamisha wagombea wao katika uchaguzi huo huki kila mmoja akiahidi kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Dk Bunungu amewashukuru wananchi wa Peramiho kwa imani yao, akiahidi kuwa mwakilishi wa wote bila kujali itikadi zao za kisiasa.
Amesisitiza kuwa, atashirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni zinatekelezwa kwa vitendo.