Tabora. Mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na saa chache baada ya kuzaliwa, ametupwa kichakani eneo ya Ipilili, Kata ya Nzega Magharibi, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, akiwa amefungwa kwenye kiroba.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi leo Februari 27, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amethitibisha kutokea kwa tukio hilo, akisema wanaendelea kumtafuta mzazi aliyefanya unyama huo.
Amesema mtoto huyo mwenye jinsi ya kiume, amekutwa katika kichaka hicho akiwa anahangaika ndani ya mfuko aina kiroba, ndipo akaokotwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Nzega Mjini na baadaye hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.
Abwao amesema mtoto huyo alitumbukizwa ndani ya mfuko na mzazi huyo akavizia muda ambao hakuna mtu anayepita katika eneo hilo, ndipo akatupwa kwenye kichaka hicho ambacho kiko kando ya barabara.
“Tunaendelea kufuatilia kujua nani ametupa kichanga hicho ili kujua changamoto ni nini mpaka afanye hivyo, na kama ni msaada apate, lakini kama ni makusudi basi hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria,” amesema kamanda huyo.
Amesema mtoto huyo anaendelea na uchunguzi wa afya yake katika Hospitali ya Nzega mkoani Tabora ili kubaini kama atakua na shida za kiafya katika kuzaliwa kwake au kutokana na mazingira aliyokutwa ili apate matibabu haraka.
“Kwa sasa mtoto huyu yuko vizuri na amezaliwa na afya njema kwa mwonekano, hivyo tunasubiri maelezo ya madaktari endapo watabaini changamoto yoyote kwenye afya yake ili apatiwe matibabu,” amesema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Ipilili wilayani humo, Said Abdallah amesema wakati akiwa na safari zake, akipita katika njia ambayo kuna kichaka, aliona kiroba kinachezacheza na baada ya kukifungua, akaona mtoto mchanga ambaye kitovu chake kilikuwa bado kibichi, ikiashiria kuwa alikuwa amezaliwa muda mfupi uliopita.
“Niliona kando ya njia kuna kiroba lakini kinasogeasogea, sasa nikasema nihakikishe kuwa ni kitu gani, ndipo nikafungua na kuona mtoto, ndiyo kama katoka kuzaliwa kwani kitovu chake hata hakijakatwa bado,” amesema mwenyekiti.
Aidha, ameomba mama aliyetupa kichanga hicho ajitokeze ili mtoto huyo apate haki ya malezi kwa sababu kitendo kilichofanywa sio kizuri kwa mtoto mdogo kiasi hicho.
“Kina mama wajitahidi kuangalia mbinu mbadala ya kutafuta malezi ya watoto wanaowazaa endapo wao hawataki kuwalea kwa sababu kitendo cha kutupa mtoto sio haki, vipi kama jamii tusingemuona, maana yake angeweza kupoteza maisha,” ameongeza.