Arusha. Mahakama ya Rufani imebariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyohukumiwa Sami Kisenga baada ya kukutwa na hatia ya kumuua shangazi yake, Holo Kisenga (50) kwa kumkata na panga kichwani na shingoni, akimtuhumu kuwa ni mchawi na amemuua baba yake.
Mauaji hayo yalidaiwa kutokea Mei 19, 2019 katika Kijiji cha Nyaligongo, Mkoa wa Shinyanga.
Sami alishtakiwa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Desemba 23, 2023.
Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa ambao ni Shaban Lila, Issa Maige na Latifa Mansoor walitoa hukumu hiyo Februari 25, 2026 na nakala ya hukumu hiyo kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Jaji Mansoor amesema Mahakama baada ya kupitia mwenendo na hoja za pande zote mbili za rufaa imekiri kuwa, upande wa mashtaka ulithibitisha bila shaka kwamba mrufani alimuua marehemu kwa kumkata kwa panga kichwani na shingoni.
Awali, katika kesi ya msingi, upande wa jamhuri uliwasilisha mashahidi sita na vielelezo vitano.
Kifo hicho kilithibitishwa na shahidi wa kwanza Dk Richard Okwachi, aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu, Mei 14 2019 ambapo alidai chanzo cha kifo hicho ni kutokana na upotevu wa damu uliosababishwa na majeraha aliyopata.
Shahidi wa pili ambaye ni mtoto wa marehemu Selemani Luchanganya, alidai kumwona mrufani akimshambulia marehemu kwa panga, shingoni na kichwani.
Alidai alikuwa na tochi, hivyo aliweza kumtambua mrufani aliyekuwepo eneo la tukio na kuwa baba yake Luchanganya Luhemeja pia alijeruhiwa alipokuwa wakijaribu kuingilia kati, hali iliyomlazimu kupiga kelele kuomba msaada na kutoka nje.
Shahidi wa tatu, Nhale Masumbuko, alidai kusikia kelele akakimbilia kutoa msaada ila alikuta Holo ameshafariki huku akiwa na jeraha kubwa shingoni.
Shahidi wa nne ambaye ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mwakitolylo, Samson Mtonja, alidai kuona mwili wa marehemu ukiwa na majeraha makubwa shingoni na kichwani na alipomuhoji mrufani alikiri mbele yake kwamba, alimuua marehemu kwa tuhuma za uchawi na kudai alimroga baba yake na kumuua.
Katika utetezi wake, mrufani alidai siku na tarehe ya tukio alikuwa katika Kijiji cha Masumbwe akihudumia shamba lake la mpunga na kudai alikamatwa Mei 20, 2019.
Alidai aliteswa na polisi, waliomlazimisha kukiri na kukubali kusaini maelezo ya onyo na kuwa hakuwa na kinyongo na shangazi yake.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote Mahakama Kuu ilisema kuwa kesi ya upande wa mashtaka ilithibitishwa bila shaka yoyote kwa kuwa, kulikuwa na ushahidi wa moja kwa moja, hivyo mrufani alihukumiwa na kuhukumiwa kifo kwa kunyongwa.
Katika rufaa yake, mrufani huyo aliibua hoja tano, zikiwamo kupinga uhalali wa ripoti ya daktari, kupinga kukubalika kwa maelezo yake ya nje ya Mahakama na kudai kuwa, maelezo hayo ya onyo yalichukuliwa nje ya muda wa kisheria.
Baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili na kupitia kwa kina ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu, wamebaini masuala makuu matatu ya kuamuliwa katika rufaa hiyo ambayo ni iwapo taarifa ya ziada ya Mahakama (ungamo la nje ya mahakama) ilirekodiwa kinyume cha Miongozo ya Jaji Mkuu.
Kuhusu hoja ya ukiukwaji wa kipengele cha sita cha Miongozo ya Jaji Mkuu, wameridhika kwamba masharti yaliyowekwa humo ni ya kiutawala na si ya lazima kwa maana ya kuathiri uhalali wa ungamo lililorekodiwa.
“Neno ‘kawaida’ lililotumika katika kipengele hicho halileti sharti la lazima bali linaelekeza utaratibu wa kawaida wa kiutendaji. Muhimu zaidi, Jaji wa Amani alizingatia kikamilifu hatua zote muhimu za kuhakikisha kuwa ungamo lilitolewa kwa hiari, bila shinikizo, ahadi au vitisho, na kwamba mrufani alifahamu madhara ya kisheria ya kauli yake. Hivyo, tunashikilia kwamba ungamo la nje ya Mahakama (kielelezo cha pili) lilikubaliwa ipasavyo na Mahakama ya Kuu,”
Amesema katika shauri hilo wamebaini maelezo ya onyo wamebaini kwamba yanaungwa mkono na ushahidi wa shahidi wa pili aliyemwona mrufani akimshambulia marehemu kwa panga, ungamo la mdomo alilolitoa mrufani mbele ya shahidi wa pili pamoja na ungamo la nje ya Mahakama lililorekodiwa kwa kufuata taratibu.
Amesema mkusanyiko wa ushahidi unathibitisha kwa kiwango cha kuridhisha ukweli wa maelezo ya onyo yaliyofutwa.
Aidha, kuhusu hoja kwamba kosa halikuthibitishwa bila shaka yoyote, wamebaini kuwa kulikuwa na ushahidi wa moja kwa moja wa kushuhudia tukio, ushahidi wa kitabibu uliothibitisha chanzo cha kifo, pamoja na maungamo ya mrufani yaliyotolewa mara tatu katika mazingira tofauti.
Jaji Mansoor amesema silaha iliyotumika, sehemu za mwili zilizolengwa na maelezo ya mrufani mwenyewe kuhusu tuhuma za uchawi kwa jumla wameridhika kwamba upande wa mashtaka ulithibitisha vipengele vyote vya kosa la mauaji.
“Kwa sababu hizo, rufaa hii haina msingi na inatupiliwa mbali,hukumu ya Mahakama Kuu inathibitishwa pamoja na adhabu iliyotolewa,” amesema.