Ushindi wampa jeuri Ndayiragije | Mwanaspoti

USHINDI mtamu nyie. Baada ya TRA United kupata ushindi wa mabao 4-1 mbele ya Fountain Gate, kocha mkuu wa timu hiyo, Etienne Ndayiragije amesema matokeo hayo yametoa majibu ya kile alichokuwa anakifanyia kazi uwanja wa mazoezi kwa safu ya ushambuliaji na sasa anarudi kuanza na safu ya ulinzi ili kupunguza uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Ndayiragije baada ya kuanza na kuipeleka TRA United hatua ya 32 bora Kombe la Shirikisho la CRDB, akiiongoza timu hiyo kushinda bao 1-0 dhidi ya Rhino Rangers.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ndayiragije alisema hawakuwa na mechi rahisi dhidi ya Fountain Gate kutokana na mpango wa wapinzani kucheza kwa kumiliki mpira, lakini mbinu sahihi alizotumia zimeamua matokeo ya juzi kwenye Uwanja wa Black Rhino, Karatu mkoani Arusha ambao Fountain wanautumia kama uwanja wao wa nyumbani.

“Timu haikuwa na wakati mzuri kwenye mechi za ligi tumepoteza mfululizo nikapata maswali ya kukiuliza kupitia michezo hiyo sasa nafurahia vijana kuweza kufanyia kazi kile tulichofundishana uwanja wa mazoezi nawapongeza,” alisema Ndayiragije na kuongeza;

“Tumefanikiwa kuondoa changamoto ya kushindwa kutumia nafasi sasa narudi uwanja wa mazoezi kuhakikisha nazungumza vizuri na safu ya ulinzi pia inapunguza makosa ilo ushindi uendane na ubora katika nafasi zote.”

Kocha huyo raia wa Burundi aliyewahi kuzinoa Mbao FC na KMC na Taifa Stars, alisema bado ana kazi ya kufanya kuhakikisha anaijenga timu hiyo kurudi katika ushindani baada ya changamoto ya matokeo mabaya ikipoteza michezo miwili mfululizo kwa idadi kubwa ya mabao.

“Tulikubali kufungwa mechi mbili mfululizo dhidi ya Mbeya City 2-0, Dodoma Jiji ilitufunga mabao 3-0, hayakuwa matokeo mazuri kwetu tumejiuliza na kufanyia kazi mapungifu tumerudi imara na kushinda mechi mbili mfululizo hili halitufanyi tukaamini tumefanikiwa bado tunahitaji kupambana zaidi ili tuwe bora.”

TRA United ipo nafasi ya 11 katika msimamo baada ya kucheza mechi 13, imeshinda michezo minne, sare nne na vipigo vitano na kufanikiwa kukusanya pointi 16 imefunga mabao 15 na kuruhusu nyavu zake kutikishwa mara 15.