Wanawake waitwa kupata msaada kuhusu ardhi

Dar es Salaam. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imewaita wanawake wote kwenye kliniki maalumu ya ardhi ‘Samia Ardhi Kliniki’ ili kupata msaada wa kitalaamu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu ardhi.

Naibu katibu mkuu wa wizara hiyo, Lucy Kabyemera amesema Samia Ardhi Kliniki itaanza Machi 2 hadi 7, 2026 katika mikoa yote 26 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka.

Kabyemera ameeleza hayo leo, Ijumaa Februari 27,2027 wakati akizungumza na wanahabari jijjini Dar es Salaam, akisema kauli mbiu ya kliniki hiyo ni: “Mwanamke, haki yako, miliki ardhi sasa.”

Amesema kliniki hiyo ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, aliyetaka wananchi kupewa huduma bora, lakini pia watumishi wa umma kutoka ofisini na kuwafuata walipo ili kuwasogezea huduma.

“Kupitia kliniki hii itakayoongozwa na watumishi wa wizara wanawake walioko katika mikoa 26, inakusudia kutoa elimu kuhusu haki ya umiliki wa ardhi kwa wanawake, kutoa msaada wa kitalaamu wa masuala ya ardhi na kutoa hatimiliki kwa waliofikia hatua ya umilikishwaji.

“Hii ni hatua mojawapo ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 (tolea la mwaka 2023) iliyozinduliwa rasmi na Rais Samia Machi 17,2025,” amesema Kabyemera.

Kabyemera amewataka wanawake nchini kujitokeza katika kliniki hizo ili kupata elimu kuhusu haki na misingi yao ya kumiliki na usimamizi wa ardhi.

“Lakini pia kutakuwa na huduma mbalimbali zinazohusu sekta ya ardhi ikiwamo kupata haki miliki papo hapo. Kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam huduma zitatolewa katika jengo la wizara,” ameeleza.

Kabyemera amesema baadhi ya mikoa kutakuwa na zaidi ya kituo kimoja kitakachotoa huduma hiyo na utaratibu maalumu utatolewa kuhusu mchakato huo.

Naibu Mkuu huyo, amefafanua kuwa Singida ndio mkoa unaongoza kwa wanawake wanaomiliki ardhi kwa asilimia 48, akisema hata Dar es Salaam inafanya vizuri kwa asilimia zaidi ya 30.

Hata hivyo, Kabyemela amesema takwimu zinaonesha wastani wa asilimia 28 ya wanawake wote ndio wanaomiliki ardhi kwa upande wa Tanzania Bara.

Katika hatua nyingine, Kabyemera amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kwa jitihada anazozifanya za kutatua migogoro ya ardhi mkoani humo.

Februari 13,2026 Chalamila alifanya ziara Manispaa ya Kinondoni kwa lengo la kusikiliza kero na kutatua migogoro ya ardhi na kubainisha kuwa chanzo cha changamoto hiyo ni tamaa, udanganyifu na matumizi ya watu wanaojifanya mawakili au madalali wanaopotosha wananchi.